AMERICAN AFFILIATE SPACE YAZINDULIWA KATIKA MAKTABA YA MKOA WA DODOMA
24 Apr, 2025
Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mhe. Omary Kipanga amezindua Kituo cha Wamerekani (American Affiliate Space) katika Maktaba ya Mkoa wa Dodoma tarehe 29 Mei, 2024.
Akizungumza katika Ufunguzi huo, Mhe. Kipanga amemshukuru Balozi wa Marekani nchini Tanzania Mhe. Dkt. Michael Battle na ujumbe wake kwa kuchagua Dodoma na Maktaba ya Mkoa wa Dodoma kuanzisha kituo hicho. Aidha ameongeza kuwa, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia chini ya Serikali ya Awamu ya Sita imejitolea kuimarisha fursa za elimu kwa Watanzania, na kusisistiza kituo hicho cha Wamarekani kitatoa fursa nyingi za elimu, maarifa na teknolojia kwa wanafunzi, watafiti na Watanzania wote.
Awali katika hotuba yake, Mhe. Kipanga alieleza kuwa kuanzishwa kwa kituo hicho Dodoma ni kielelezo cha kuheshimiana na uwepo wa urafiki wa muda mrefu kati Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baba wa Taifa Hayati Mwl. J.K. Nyerere na Hayati Rais John F. Kennedy wa Marekani miaka mingi iliyopita.
Kwa upande mwingine, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mhe. Jabiri Shekimweri, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, ameushukuru Ubalozi wa Marekani kwa hatua walioichukua kufungua Kituo hicho, huku akiwataka wanafunzi, watafiti, vyombo vya habari na Watanzania wote kutumia kituo hicho kwa kujipatia taarifa mbalimbali na kuahidi kutunza miundombinu na vifaa vyote vilivyomo kwa kushirikiana na TLSB ili Watanzania wazidi kunufaika na huduma hizo kwa muda mrefu bila kikwazo chochote.
Naye Balozi wa Marekani Nchini Tanzania Mhe. Dkt. Michael Battle, amemshukuru Naibu Waziri Mhe. Omary Kipanga kwa kwa ushauri wake juu ya kuanzishwa kwa Kituo cha Wamerekani katika Maktaba ya Mkoa wa Dodoma. Vilevile ameishukuru Menejimenti na Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania kuridhia kutoa nafasi kwenye Maktaba ya Mkoa wa Dodoma ili kituo hicho kianzishwe.
Mhe. Dkt. Battle, ameeleza kuwa juhudi za Serikali kukamilisha kuhamisha Makao Makuu ya Nchi jijini Dodoma ifikapo 2025, kumewafanya nao kuanzisha Ubalozi wa Marekani Jijini Dodoma na kusisitiza Kituo cha Wamarekani katika Maktaba ya Mkoa wa Dodoma kimeongeza idadi ya Vituo hivyo nchini, ambapo kwasasa kuna vituo Pemba, Mwanza, Dar es Salaam na Zanzibar.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TLSB Dkt. Mboni Ruzegea, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za kuendelea kuimarisha fursa za elimu kwa Watanzania nchini bila kusahau kuimarisha huduma za Maktaba. Aidha ameushukuru Uongozi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Ubalozi wa Marekani nchini kwa kuanzisha kituo hicho chenye vifaa mbalimbali vya teknolojia ya kisasa ambavyo vitasaidia Watanzania na watumiaji wa Maktaba kujifunza, kujipatia taarifa mbalimbali na kutanua wigo wao wa Maarifa na teknolojia katika nyanja mbalimbali.
Vituo vya Wamarekani (American Affiliate Spaces) hutumika kutoa huduma mbalimbali kama kumbi za mihadhara, warsha na maonesho mbalimbali. Vilevile, vinakuza ujuzi wa kidijitali, ufikiaji wa teknolojia na rasilimali za kidigitali.