Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania

TLSB Logo TLSB Logo
Tafuta kwenye kwa
NAIBU KATIBU MKUU WIZARA YA ELIMU ATEMBELEA TLSB, APONGEZA HATUA ZA MABORESHO YA HUDUMA ZA MAKTABA KIDIJITALI
04 Aug, 2025
service image
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Hussein Mohamed Omar, ametembelea Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB) katika Makao Makuu yake yaliyopo Dar es Salaam leo tarehe 22 Julai, 2025, kwa lengo la kujionea, kujifunza na kupata uelewa wa kina kuhusu shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Bodi hiyo. Ziara hiyo imefanyika ikiwa ni takribani mwezi mmoja tangu Dkt. Omar ateuliwe kushika wadhifa huo, ikiwa ni sehemu ya jitihada zake za kuzijua taasisi zilizo chini ya Wizara pamoja na mchango wake katika maendeleo ya sekta ya elimu nchini. Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Dkt. Omar amesema kuwa lengo kuu la kutembelea TLSB ni kuifahamu Bodi kwa undani, majukumu yake ya msingi pamoja na mchango wake katika kukuza elimu, maarifa na utamaduni wa kujisomea kwa Watanzania. Ameeleza kuwa katika kipindi hiki ambacho Serikali inaendelea kuhimiza matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma kwa wananchi, taasisi kama TLSB zina nafasi kubwa ya kuhakikisha maarifa yanawafikia wananchi wengi zaidi kwa njia rahisi na jumuishi. Katika hatua nyingine, Naibu Katibu Mkuu huyo aliipongeza TLSB pamoja na Menejimenti yake kwa hatua kubwa iliyofikiwa katika maandalizi ya utoaji wa huduma za maktaba kwa njia ya mtandao, kupitia Maktaba Mtandao Jumuishi ya Kitaifa, ambayo ipo katika hatua za mwisho za maandalizi kuelekea uzinduzi rasmi. “Nitumie fursa hii kuwapongeza sana Bodi na Menejimenti kwa hatua mliyofikia kuelekea utoaji wa huduma za maktaba kidijitali. Hatua hii itawezesha wananchi wengi zaidi, hususan wanaoishi pembezoni mwa miji na maeneo ya vijijini, kupata huduma za maktaba kwa urahisi, kuchochea utamaduni wa kujisomea na kuongeza upatikanaji wa maarifa kwa maendeleo ya mtu binafsi na taifa kwa ujumla,” amesema Dkt. Omar. Aidha, Dkt. Omar ameeleza dhamira ya Wizara kushirikiana na TLSB katika kutafuta washirika wa maendeleo pamoja na miradi mbalimbali, itakayowezesha Watumishi wa Bodi kupata fursa za mafunzo na kubadilishana uzoefu nje ya nchi. Mafunzo hayo yatalenga zaidi usimamizi wa maktaba za kisasa, matumizi ya teknolojia ya hali ya juu na mifumo ya kidijitali, ili kuiwezesha TLSB kutekeleza majukumu yake kwa viwango vya kimataifa, kulingana na mahitaji ya wakati wa sasa. Awali, akitoa taarifa ya Bodi, Mkurugenzi Mkuu wa TLSB, Dkt. Mboni Ruzegea, aliwasilisha kwa Naibu Katibu Mkuu muhtasari wa majukumu ya TLSB, muundo wa kiutendaji na shughuli mbalimbali zinazotekelezwa, pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka minne kuanzia 2021 hadi 2025. Katika maelezo yake, Dkt. Ruzegea aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuipa kipaumbele sekta ya maktaba nchini kupitia utekelezaji wa hatua mbalimbali za kimkakati, ikiwemo: Ujenzi na ukarabati wa majengo ya maktaba katika maeneo mbalimbali nchini; Uanzishaji wa Maktaba Mtandao Jumuishi ya Kitaifa ili kuongeza upatikanaji wa huduma za maktaba kidijitali kwa wananchi; Ununuzi wa vifaa vya TEHAMA kwa ajili ya kuboresha utoaji wa huduma; Maboresho ya sheria na miongozo inayosimamia huduma za maktaba nchini; Ongezeko la Bajeti ya TLSB ili kuimarisha utekelezaji wa majukumu yake; Ongezeko la Watumishi kupitia ajira mpya, hatua iliyoongeza ufanisi katika utoaji wa huduma; Utekelezaji wa mradi wa ununuzi wa vitabu vitakavyosambazwa katika maktaba za jamii nchini; Kuanzishwa kwa kozi mpya chuoni SLADS, zitakazosaidia kuongeza idadi na ubora wa wataalamu wa maktaba nchini. Katika kuhitimisha ziara yake, Naibu Katibu Mkuu alitembelea Divisheni na Vitengo mbalimbali vya TLSB, ambapo alipata maelezo ya moja kwa moja kuhusu utekelezaji wa majukumu ya kila kitengo, changamoto zinazokabiliwa na mipango ya baadaye. Vilevile, alifanya kikao cha pamoja na Watumishi wa TLSB, akisisitiza umuhimu wa uwajibikaji, ubunifu, mshikamano na matumizi ya teknolojia katika kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi. Ziara hiyo imeelezwa kuwa ni kichocheo muhimu cha kuimarisha ushirikiano kati ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na TLSB, pamoja na kuipa Bodi motisha zaidi katika kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kusimamia, kuratibu na kuendeleza huduma za maktaba nchini, kwa manufaa ya jamii na maendeleo ya taifa kwa ujumla.