DKT. MBONI RUZEGEA AFUNGUA MAONESHO YA VITABU YA MELI YA KIMATAIFA YA LOGOS HOPE
24 Apr, 2025
Mkurugenzi Mkuu wa TLSB Dkt. Mboni Ruzegea, amefungua maonesho ya vitabu yaliyofanyika katika Meli ya kimataifa ya LOGOS HOPE iliyotia nanga katika bandari ya Dar es Salaam, Ghati namba 2, tarehe 6 Oktoba, 2023.
Akimuwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Carolyne Nombo kwenye ufunguzi wa maonesho hayo, Dkt. Ruzegea katika hotuba yake amesema kuwa amefurahishwa sana na ujio wa Meli ya LOGOS HOPE nchini pamoja na watendaji wake wote na kumshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia ujio wa Meli hiyo kwa manufaa ya Watanzania wote.
Dkt. Ruzegea ameongeza kuwa, maonesho hayo yenye aina ya vitabu zaidi ya elfu sita (6000) vya kada mbalimbali kama vile; Sayansi, teknolojia, Sanaa, Maarifa ya jamii, lugha, dini na mapishi kwa ajili ya familia zote, yatasaidia sana maendeleo ya mtu binafsi kwa kila atakayetembelea maonesho hayo huku akipendekeza mijadala na mikutano ya viongozi, wanaume na wanawake, vijana na watoto ifanyike katika maonesho hayo ili kuleta nguvu mpya ya mabadiliko.
Vilevile, ametumia nafasi hiyo kuyaomba mashirika na taasisi nyingine za kidini kutoa huduma kama zinazotolewa na LOGOS HOPE ili kuusaidia umma wa watanzania wanaohitaji ujuzi na maarifa mbalimbali katika maisha yao ya kila siku, huku akiamini sawasawa na jamii ya LOGOS HOPE kwamba umasikini ni mtego ambapo wanaonaswa na mtego huo hutaabika sio tu kwa uhaba wa fedha, bali pia ukosefu wa elimu na huduma za Afya zinazohitajika kuvunja duara la umasikini unaowakabili.
Aidha, Dkt. Ruzegea amewaomba wakazi wa mkoa wa Dar es Salaam, viunga vyake na mikoa yote ya jirani kutumia fursa hii ya maonesho kuja kujifunza maarifa na ujuzi mpya kutoka katika vitabu na watendaji wa LOGOS HOPE.
Kwa upande wake Mkurugenzi na kiongozi wa LOGOS HOPE Ndugu. Edward David, katika hotuba yake, amesema amefurahishwa na mapokezi ya meli hiyo na kuishukuru serikali ya Tanzania kwa kuridhia ujio wao. Vilevile amemshukuru Mgeni Rasmi kwa kutenga muda wake kufungua maonesho hayo.
Ndugu David amesema kuwa, kama lilivyo jina la Meli Hiyo LOGOS HOPE, lengo lake hasa ni kuleta tumaini jipya katika maisha ya watu duniani kote kwa kubadilishana ujuzi, maarifa na uhamasishaji wa usomaji ambapo watu zidi ya elfu tatu (3000) hutembelea Meli hiyo kila wanapotia nanga katika nchi mbalimbali duniani.
Aidha ameongeza kuwa, LOGOS HOPE hufanya pia shughuli mbalimbali za kijamii na kisamaria huku akibainisha huduma walizotoa kama vile; kuleta maridhiano baada ya vita vya kimbari katika mji wa Papua nchini Guinea, Ujenzi wa vituo vya Kulelea watoto yatima nchini Myanmar na Liberia. Ujenzi wa nyumba zilizokumbwa na maafa nchini Nicaragua na Grenada, na michango ya vitabu kwa nchi mbalimbali ikiwemo Sudan na Mashariki ya Timor.
Meli ya LOGOS HOPE inamilikiwa na taasisi ya GBA Ships ya Ujerumani na ina watendaji wapatao mia 400 kutoka mataifa mbalimbali ikiwemo Tanzania ambao hufanya shughuli ndani ya meli hiyo kwa kujitolea.
Meli hiyo ilifanya maonesho ya vitabu kwa takribani siku 18 kuanzia tarehe 6 - 22 Oktoba 2023. Muda wa maonesho ilikua ni kuanzia saa 5:00 asubuhi – 7:00 mchana (kwa Watoto na wanafunzi mpaka miaka 18) na saa 7:00 mchana – 11:30 jioni (kwa Wananchi wote) siku ya Jumatatu – Ijumaa, katika bandari ya Dar es Salaam, Ghati namba 2 kwa kiingilio cha shilingi elfu moja (1000) kwa mtu mmoja.