DKT. MBONI RUZEGEA AKUTANA NA WATUMISHI WAPYA WA TLSB, AWASISITIZA UADILIFU, NIDHAMU NA UWAJIBIKAJI
31 Aug, 2026
31 Agosti 2026
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB), Dkt. Mboni Ruzegea, leo tarehe 31 Agosti 2026 amekutana na watumishi wapya 23 wa kada ya Ukutubi katika kikao cha ‘induction’ kilichofanyika katika Ukumbi Mkuu wa Mikutano wa TLSB, Makao Makuu jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kuwajengea uelewa kuhusu majukumu yao na matarajio ya taasisi kwa watumishi hao.
Katika kikao hicho, Dkt. Ruzegea amesisitiza kuwa muda wa kazi ni jambo la msingi kuliko yote, akiwataka watumishi hao kuutumia vyema muda wao kwa kufanya kazi kwa bidii, kujituma na kuhakikisha wanatoa mchango wenye tija kwa taasisi na taifa. Amesema kuwa, kwa kuwa wengi wao bado wana umri mdogo ukilinganisha na miaka mingi wanayotarajiwa kuitumikia Serikali, wanapaswa kutumia kipindi hicho kujenga misingi imara ya utendaji na kulitumikia taifa kwa ufanisi.
Aidha, amewasisitiza kuwa na uadilifu, nidhamu, ubunifu na heshima kwa viongozi, pamoja na kuwa sehemu ya utatuzi wa changamoto za taasisi badala ya kuwa chanzo cha changamoto. Amewataka kutosubiri kupangiwa kila jambo, bali kuwa na utayari wa kubaini majukumu na kuchukua hatua za kuyatekeleza kwa mujibu wa taratibu. Pia amewakumbusha umuhimu wa kujaza na kusimamia vizuri mfumo wa PEPMIS, akieleza kuwa utendaji unaoonekana kupitia mfumo huo ni sehemu muhimu ya tathmini ya utendaji na maendeleo yao ya kikazi.
Dkt. Ruzegea pia amewataka watumishi hao kuifahamu kwa kina Sheria ya TLSB (Revised) ya mwaka 2023, pamoja na kusoma na kuelewa Mpango Mkakati mpya wa TLSB wa miaka mitano ijayo, ili waweze kutambua vipaumbele vya taasisi na kuelekeza nguvu zao katika maeneo yanayochangia utekelezaji wa malengo ya TLSB. Vilevile, amewahimiza kujifunza shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na taasisi, ikiwemo kazi za Kitengo cha Bibliografia ya Taifa, Utafiti na Maktaba Mtandao.
Akihitimisha, Dkt. Ruzegea amewataka watumishi hao kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia katika sekta ya maktaba na huduma za taarifa, ikiwemo kutumia Akili Unde (AI) kwa weledi, umakini na usahihi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.


