KONA YA WATOTO TLSB YAFUNGULIWA MARA BAADA YA KUBORESHWA MUONEKANO WAKE
24 Apr, 2025
Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania imefanya Ufunguzi wa Kona ya Watoto iliyopo ndani ya jengo la Maktaba Kuu ya Taifa, jijini Dar es Salaam leo tarehe 30 Januari, 2025 mara baada ya ukarabati mdogo uliofanyika kwa kushirikiana na Shirika la Book Aid International (BAI) la Uingereza kukamilika. Ukarabati huo umehusisjha kupaka rangi na michoro mbalimbali katika Kona hiyo ili kuongeza mvuto wa mwonekano wake na kuvutia watoto wengi zaidi kujiunga na kutumia huduma za Maktaba.
Akifungua Kona hiyo, Msimamizi wa dawati la Maktaba kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Mgeni Rasmi Dkt. Maryam Mwinyi, ameupongeza Uongozi wa TLSB kwa juhudi na kazi wanayoifanya katika kuhakikisha huduma za Maktaba, miundombinu ya majengo na mifumo ya kiutendaji inaboreshwa kote nchini ili kutoa huduma kwa uweledi na ufanisi, hivyo kufikia umma wa Watanzania hasa walioko maeneo ya vijijini, sawasawa na malengo ya Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, katika kufikisha huduma za Maktaba kote nchini.
Dkt. Maryam ametumia nafasi hiyo pia kuwapongeza Book Aid International kwa ukarabati walioufanya katika kona ya watoto na kukaribisha wadau, washirika na wadhamini wengine kujitokeza kuunga mkono juhudi za Wizara na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kupeleka mbele gurudumu la maendeleo Sekta ya Elimu nchini, ikiwemo uboreshaji wa Huduma za Maktaba.
Aidha, amewataka wazazi kuhakikisha wanafuatilia vitabu na maudhui ambayo watoto wao wanasoma kama yanaendana na mila na desturi za Kitanzania na kuwaepusha na athari zinazoweza kujitokeza hasa mmonyoko wa maadili.
Awali katika taarifa yake Mkurugenzi wa Uendeshaji Huduma za Maktaba Dkt. Rehema Ndumbaro (akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu), ameeleza kuwa BAI ni wadau wa muda mrefu wa TLSB na mwaka 2024/2025 wametoa fedha kuendeleza kona ya watoto kwa mkoa wa Dar es salaam mara baada ya kuvutiwa na Ukarabati wa Jengo la Maktaba Kuu ya Taifa uliofanywa na Serikali.
Dkt. Ndumbaro ameongeza kuwa, kabla ya ukarabati huo, BAI walitoa mafunzo kwa Wakutubi yaliyolenga kuwanoa ili kutekeleza majukumu yao kwa uweledi na ufanisi, na baadae kuleta vitabu 3000 vya maudhui ya watoto vilivyoandikwa kwa lugha ya Kiingereza. Vilevile, walitoa fedha kwa kwa ajili ya ununuzi wa vitabu 1000 vya maudhui ya Kitanzania, vilivyoandikwa kwa lugha ya Kiswahili na Waandishi wa ndani.
Kwa upande mwingine, Msimamizi wa Maktaba za Mikoa Bi. Nikobiba Kigadye amewashukuru BAI kwa udhamini huo na kuwaomba wazidi kuchangia vitabu katika Maktaba za Mikoa ili kunufaisha jamii iliyoko vijijini.
Naye, Mkurugenzi wa Rasilimali watu na Utawala Bi. Veneranda Mpaze amewashukuru Mgeni Rasmi, wageni waalikwa na Watumishi wa TLSB kwa kutenga muda wao kuhudhuria Ufunguzi huo, huku akiitaka jamii kutumia Huduma za Maktaba, kwani mbali na usomaji wa Vitabu kuna huduma nyingine mbalimbali ambazo watanufaika nazo.
Ufunguzi wa Kona ya Watoto umehudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Serikali wakiwemo; ndug. Rajab Kingalawe kutoka Ofisi ya Kamishna wa Elimu WyEST, Mwakilishi wa Afisa Elimu Mkoa wa Dar es es Salaam ndug. Abeid Millanzi, Mwakilishi wa Afisa Elimu Wilaya ya Ilala ndug. Ibrahim Msingwa, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kibasila Upanga Bi. Marium Jaffar, Walimu, wanafunzi na Watumishi wa TLSB.