Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania

TLSB Logo TLSB Logo
Tafuta kwenye kwa
KONGAMANO LA KWANZA LA NDANI KUHUSU UBORESHAJI WA HUDUMA ZA MAKTABA
31 Dec, 2025
service image
Wakutubi nchini wametakiwa kubuni na kuimarisha mbinu mpya katika utekelezaji wa majukumu yao ili kutoa huduma kwa uweledi na ufanisi, hatua itakayowezesha jamii kunufaika kikamilifu na maarifa yaliyopo katika Maktaba. Wito huo umetolewa tarehe 03 Desemba, 2025 na Mratibu wa Masuala ya Maktaba kutoka Ofisi ya Kamishna wa Elimu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Maryam Mwinyi, wakati akifungua Kongamano la Kwanza la Ndani kuhusu Uboreshaji wa Huduma za Maktaba nchini, lililofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Maktaba ya Mkoa wa Ruvuma. Akizungumza katika ufunguzi wa Kongamano hilo, Dkt. Mwinyi alisema Wakutubi wana wajibu mkubwa wa kuhakikisha maarifa na ujuzi vilivyopo katika Maktaba vinasambazwa kwa jamii, badala ya kubaki kama taarifa zinazohifadhiwa bila kutumika ipasavyo. “Elimu si kujaza tu taarifa kichwani mwa mtu, bali ni kumpa maarifa yanayohitajika ili aweze kutatua changamoto zinazomkabili. Kwa kuzingatia Kauli Mbiu ya Kongamano hili isemayo ‘Jamii Yetu, Maktaba Yetu!’, nawasihi mfuatilie kwa umakini mafunzo yatakayotolewa ili myatekeleze majukumu yenu kwa uweledi na ufanisi,” amesema Dkt. Mwinyi. Aidha, Dkt. Mwinyi alieleza kuwa mafunzo yatakayotolewa katika Kongamano hilo yamelenga kujenga na kuimarisha stadi za kazi, kuongeza maarifa ya kitaaluma, pamoja na kuendeleza uongozi wenye tija miongoni mwa Wakutubi, ili kuendana na mabadiliko ya sayansi, teknolojia na mahitaji ya jamii ya sasa. Awali akimkaribisha Mgeni Rasmi, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB), Dkt. Mboni Ruzegea, alisema Kongamano hilo ni la kwanza na la kihistoria, kwani limewakutanisha Wakutubi kutoka Maktaba za Mikoa, Wilaya na Tarafa kutoka jumla ya Maktaba 43 za TLSB nchini. Dkt. Ruzegea aliwataka Wakutubi, ambao ndio walengwa wakuu wa Kongamano hilo, kutumia kikamilifu maarifa na uzoefu watakaoupata ili kujitathmini, kubaini changamoto zilizopo katika maeneo yao ya kazi, na kuweka mipango mkakati thabiti itakayosaidia kuboresha utoaji wa huduma za Maktaba kwa jamii. Kongamano la Kwanza la Ndani kuhusu Uboreshaji wa Huduma za Maktaba lilihudhuriwa pia na Wakurugenzi wa Idara, Wakuu wa Vitengo, na Wakuu wa Sehemu mbalimbali za TLSB, ambapo mada tofauti ziliwasilishwa kwa lengo la kujenga uelewa wa pamoja, kubadilishana uzoefu na kuimarisha mshikamano katika utekelezaji wa majukumu ya Maktaba nchini. Kongamano hilo lilianza rasmi tarehe 03 Desemba, 2025 na kutamatika tarehe 04 Desemba, 2025, likiwa ni jukwaa muhimu la kutafakari na kuweka mwelekeo mpya wa uboreshaji wa huduma za Maktaba ili ziendelee kuwa chachu ya maendeleo ya elimu, maarifa na jamii kwa ujumla.