MAHAFALI YA ISHIRINI NA TISA (29) YA CHUO CHA UKUTUBI NA UHIFADHI NYARAKA (SLADS)
24 Apr, 2025
Mkurugenzi wa Uendelezeji Taasisi Ofisi ya Rais, menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ndugu Nolasco Kipanda, amewatunuku Wahitimu 196 Stashahada ya Ukutubi na Uhifadhi Nyaraka ya Chuo Cha Ukutubi Na Uhifadhi Nyaraka (SLADS) katika mahafali ya 29 yaliyofanyika tarehe 25 Novemba 2023, kwenye viwanja vya Chuo hicho Wilaya ya Bagamoyo, Mkoani Pwani.
Katika hotuba yake, ndug. Kipanda amewasihi Wahitimu hao kutumia elimu waliyoipata kujiajiri huku wakiendelea kuomba nafasi mbalimbali zitakazotangazwa na serikali na sekta binafsi.
Kipanda ameongeza kuwa, ni vyema pia Wahitimu na jamii kuchukua tahadhari kuhusu magonjwa yasiyoambukiza na mpangilio mzuri wa vyakula sambamba na kufanya mazoezi ili kuweka Afya sawa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya huduma za Maktaba Tanzania (TLSB) ambaye pia ni mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha SLADS Dkt. Mboni Ruzegea amesema kuwa;
“serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeendelea kukiwezesha Chuo chetu kutimiza jukumu lake la kutoa mafunzo bora ya Ukutubi na Utunzaji Nyaraka kwa ajili ya maendeleo ya Umma wa Tanzania. Kipekee sana tunaishukuru Serikali kwa kutupatia fedha TZS. Millioni mia saba kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya kufundishia na kujifunzia kwa mwaka huu wa fedha 2023/2024.” Dkt. Ruzegea ameeleza.
Dkt. Ruzegea ameongeza kuwa, TLSB kupitia Chuo chake cha SLADS itaendelea kuhakikisha kuwa inaendelea kuwajengea vijana uwezo na msingi imara kwa ajili ya maendeleo ya jamii na maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
Naye Mkuu wa Chuo cha SLADS Dkt. Alfred John Nchimbi amesema kuwa, katika kutekeleza maelekezo ya serikali ya kuzalisha wahitimu wenye ujuzi unaowawezesha kuajiriwa na kujiajiri, Chuo kimekamilisha zoezi la kufanya rejea ya mitaala yake kwa kuzingatia viwango vya ubora vya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi (NACTVET)
“Kupitia zoezi hilo chuo kimeongeza moja ya Kozi ambayo ni Utunzaji Kumbukumbu yaani ‘’Records Management’’. Chuo kimejipanga kuongeza idadi ya kozi zinazotolewa chuoni kulingana na mahitaji ya jamii na ukuaji wa miundombinu ya kufundishia na kujifunzia.” Dkt. Nchimbi amebainisha.
Katika Risala yao kwa Mgeni Rasmi, Wahitimu walitoa shukrani zao za dhati kwa Elimu waliyoipata Chuoni hapo na kuahidi kwenda kulitumikia vyema taifa, huku wakitanabaisha changamoto mbalimbali zinazohitaji ufumbuzi kwa mustakabali na ustawi wa Chuo hicho.
Chuo cha Ukutubi na Uhifadhi Nyaraka kilianzishwa mwaka 1989 chini ya Sheria ya Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania ya mwaka 1975. Kabla ya kuanzishwa kwa Chuo hicho, BOHUMATA ikishirikiana na Wizara ya Elimu wakati huo ilianzisha mafunzo ya Ukutubi kwa ngazi ya Cheti mwaka 1972, katika majengo ya Chuo cha Ualimu Dar es Salaam (Chang’ombe) na mwaka 1975 mafunzo hayo yalihamishiwa majengo ya Maktaba Kuu ya Taifa. Mafunzo ya Ukutubi kwa ngazi ya Stashahada yalianzishwa na kuunganishwa na yale ya Cheti mwaka 1989 katika majengo ya Chuo cha Uongozi wa Elimu MANTEP kwa sasa ADEM. Mwaka 2008 mafunzo yalihamishiwa eneo la Ukuni baada ya Chuo kupata majengo yake. Kwa sasa Chuo kina kampasi mbili: Bagamoyo ambayo ndiyo makao makuu na kampasi ya Dar es Salaam iliyopo ndani ya majengo ya Maktaba Kuu ya Taifa. Chuo kinatoa Kozi ya Ukutubi na Uhifadhi Nyaraka kwa ngazi tatu:
Mafunzo ya Awali ya Ukutubi (Basic Technician Certificate)
Mafunzo ya Cheti (Technician Certificate)
Mafunzo ya Stashahada (Ordinary Diploma)
Vilevile kwasasa Chuo kimeanzisha Kozi mpya ya Utunzaji Kumbukumbu yaani ‘’Records Management’’ baada ya mapitio ya Mitaala Mipya. Chuo pia huendesha kozi fupi kulingana na mahitaji maalum kwa Watumishi kutoka Serikalini na Sekta binafsi.