WAJUMBE WA KAMATI ZA BARAZA LA WAWAKILISHI ZANZIBAR WATEMBELEA TLSB KUJIFUNZA UENDESHAJI WA HUDUMA ZA MAKTABA
02 Sep, 2026
Wajumbe wa Kamati za Baraza la Wawakilishi Zanzibar, ikiwemo Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) na Kamati ya Ustawi wa Jamii, pamoja na viongozi kutoka Wizara ya Elimu, Mafunzo ya Amali Zanzibar (WEMA) na wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia (WyEST) wametembelea Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB) kwa lengo la kujifunza namna Bodi inavyotekeleza majukumu yake na kutoa huduma za maktaba nchini.
Ziara hiyo imefanyika leo, Septemba 2, 2026, katika Maktaba Kuu ya Taifa jijini Dar es Salaam, ambapo ujumbe huo uliongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali, Mhe. Kombo Mwinyi Shehe, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Ustawi wa Jamii na Mhe. Dkt. Nasser Nassir Omari Naibu na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe. Khadija Salum Aly,
Katika ziara hiyo, wajumbe walipata fursa ya kutembelea vitengo mbalimbali vya Maktaba Kuu ya Taifa na kujionea kwa vitendo namna huduma za maktaba zinavyotolewa. Vitengo vilivyotembelewa ni pamoja na Kitengo cha Huduma za Usomaji kwa Watu Wazima (RSD), Kitengo cha Ufundi (TSD), Kitengo cha Bibliografia ya Taifa (NBA) na Kitengo cha Watoto na Shule (CSSD).
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TLSB, Dkt. Mboni A. Ruzegea, aliwasilisha taarifa ya Bodi na kueleza namna TLSB inavyotekeleza majukumu yake katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za maktaba na taarifa, sambamba na kuchangia utekelezaji wa vipaumbele vya maendeleo ya Dira ya Taifa 2050.
Dkt. Mboni alieleza kuwa TLSB inaendelea kuimarisha huduma zake kwa kuendana na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya jamii, huku ikilenga kuhakikisha huduma za maktaba zinakuwa jumuishi, rahisi kufikiwa na zenye tija kwa wananchi.
Aidha, alieleza kuwa mfumo wa INDLS (Integrated National Library System) ni miongoni mwa hatua muhimu katika mageuzi ya huduma za maktaba nchini, kwa kuwa utasaidia kuunganisha huduma mbalimbali za maktaba na kuwawezesha wasomaji, waandishi na wachapishaji kupata huduma kwa urahisi zaidi kupitia mfumo wa kidijitali.
Aliongeza kuwa mfumo huo utarahisisha pia taratibu za usajili na upatikanaji wa huduma zinazohusiana na namba tambulishi za machapisho, ikiwemo ISBN na ISSN, hivyo kupunguza changamoto za kimfumo na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali, Mhe. Kombo Mwinyi Shehe, pamoja na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Ustawi wa Jamii, Mhe. Dkt. Nasser Nassir Omari, waliishukuru TLSB kwa mapokezi mazuri na kwa kuwapatia uelewa mpana kuhusu namna Bodi inavyotekeleza majukumu yake katika maeneo mbalimbali nchini.
Walisema ziara hiyo imewapa fursa ya kujifunza uzoefu unaoweza kusaidia kuboresha na kuimarisha huduma za maktaba na upatikanaji wa taarifa, hususan katika mazingira ya mabadiliko ya teknolojia na ongezeko la mahitaji ya huduma za kidijitali.
Naye Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe. Khadija Salum Aly, ameishukuru TLSB kwa kushirikiana na ujumbe huo na kutoa fursa ya kujifunza uzoefu wa uendeshaji wa huduma za maktaba.
Mhe. Khadija amesema uzoefu walioupata kupitia ziara hiyo utakuwa chachu ya kuboresha huduma za maktaba katika taasisi za elimu Zanzibar, huku akiahidi kuendeleza na kuimarisha ushirikiano kati ya TLSB na Bodi ya Huduma za Maktaba Zanzibar (ZLSB) kwa lengo la kuongeza ufanisi wa huduma za maktaba na taarifa kwa wananchi wa pande zote mbili.
Aidha Wajumbe walpata wasaa wa kuuliza maswali,kutoa maoni na kujibiwa na mkurugenzi mkuu wa TLSB.


