SLADS ALUMNI WAKABIDHI KOMPYUTA MPAKATO 11 SLADS
31 Dec, 2025
Umoja wa Wahitimu wa Chuo cha Ukutubi na Uhifadhi Nyaraka (SLADS ALUMNI) umekabidhi jumla ya Kompyuta Mpakato 11 kwa Chuo cha Ukutubi na Uhifadhi Nyaraka (SLADS) katika hafla iliyofanyika tarehe 20 Desemba, 2025.
Hafla hiyo ya makabidhiano ilifanyika mbele ya viongozi mbalimbali wa Serikali na Menejimenti ya SLADS, ambapo kompyuta hizo zilikabidhiwa rasmi ili kusaidia kuimarisha mazingira ya kujifunzia, hususan katika Maabara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) chuoni hapo.
Akikabidhi kompyuta hizo kwa niaba ya SLADS ALUMNI, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Mhe. Shaibu Ndemanga, aliipongeza Jumuiya hiyo kwa moyo wa uzalendo waliouonesha kwa Chuo chao, akibainisha kuwa mchango huo ni wa mfano na unaopaswa kuungwa mkono na jamii nzima. Alisema kompyuta hizo zitasaidia kwa kiwango kikubwa kuboresha ujifunzaji kwa wanafunzi wanaoendelea na masomo katika Chuo cha SLADS.
Mhe. Ndemanga aliongeza kuwa katika kipindi cha sasa, teknolojia imekua kwa kasi kubwa, hivyo uwepo wa vifaa vya TEHAMA kama kompyuta mpakato utawawezesha wanafunzi kwenda sambamba na maendeleo ya teknolojia katika masuala ya uandaaji, uhifadhi na utunzaji wa taarifa na nyaraka. Aidha, katika kuunga mkono juhudi za SLADS ALUMNI, Mhe. Ndemanga aliahidi kuchangia kompyuta mpakato 10 zaidi kwa Chuo cha SLADS ili kuendelea kuimarisha miundombinu ya TEHAMA.
Akipokea kompyuta hizo kwa niaba ya Chuo, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha SLADS ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB), Dkt. Mboni Ruzegea, aliwashukuru kwa dhati SLADS ALUMNI kwa mchango huo muhimu. Alieleza kuwa kitendo hicho kinaonesha upendo, mshikamano na kuthamini taasisi iliyowajengea msingi wa taaluma, na kuitaka jamii pamoja na wadau wengine wa elimu kuiga mfano huo kwa kuchangia maendeleo ya taasisi za elimu nchini.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa SLADS ALUMNI, Bi. Flora Joseph Ondi, alisema kuwa uamuzi wa kununua na kukabidhi kompyuta mpakato hizo umetokana na changamoto walizowahi kukutana nazo wakati wakisoma katika Maabara ya TEHAMA chuoni hapo. Alibainisha kuwa SLADS ALUMNI waliona umuhimu wa kuchangia vifaa hivyo ili kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi waliopo sasa.
Bi. Ondi aliongeza kuwa mchango huo pia ni sehemu ya shukrani kwa Chuo cha SLADS na TLSB kwa mafunzo bora waliyowapatia wahitimu hao, na kuahidi kuwa SLADS ALUMNI wataendelea kukisaidia Chuo hicho kadiri ya uwezo wao kwa lengo la kuendeleza taaluma ya Ukutubi na Uhifadhi Nyaraka pamoja na kuchangia maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM), Dkt. Maulid Maulid, pamoja na Kaimu Mkuu wa Chuo cha SLADS, Bi. Bertha Mwaihojo, ambao walishuhudia zoezi hilo na kupongeza ushirikiano mzuri kati ya Chuo na Wahitimu wake.
Pichani: Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Mhe. Shaibu Ndemanga (katikati) akikabidhi Kompyuta Mpakato kwa Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha SLADS na Mkurugenzi Mkuu wa TLSB, Dkt. Mboni Ruzegea (kushoto). Kulia ni Bi. Flora Joseph Ondi, Mwakilishi wa SLADS ALUMNI, akishuhudia tukio hilo pamoja


