Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania

TLSB Logo TLSB Logo
Tafuta kwenye kwa
SLADS NA ADEM KUTOA MAFUNZO YA MUDA MFUPI KWA WATENDAJI SEKTA YA ELIMU
31 Dec, 2025
service image
Chuo cha Ukutubi na Uhifadhi Nyaraka (SLADS) kwa kushirikiana na Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) wameingia katika Mkataba wa Makubaliano ya Kazi (MoU) unaolenga kuimarisha utoaji wa Mafunzo ya Muda Mfupi kwa Watendaji na Watumishi wa sekta ya Elimu nchini Tanzania. Mkataba huo ulisainiwa rasmi tarehe 20 Desemba, 2025, katika Ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Stella Maris Maris, Bagamoyo, Mkoa wa Pwani. Hafla hiyo ilifanyika mbele ya Vyombo vya Habari pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali na taasisi za elimu. Kwa upande wa SLADS, mkataba huo ulisainiwa na Kaimu Mkuu wa Chuo, Bi. Bertha Mwaihojo, huku upande wa ADEM ukisainiwa na Mtendaji Mkuu wa Wakala huo, Dkt. Maulid Maulid. Makubaliano hayo yanatarajiwa kuwezesha taasisi hizo mbili kushirikiana katika kubuni, kuandaa na kutoa mafunzo ya muda mfupi yatakayolenga kuwaongezea ujuzi wa kitaaluma, kiutendaji na kiuongozi Watendaji na Watumishi wa sekta ya Elimu nchini. Akizungumza baada ya utiaji saini, Bi. Bertha Mwaihojo alisema kuwa ushirikiano huo ni hatua muhimu kwa SLADS katika kutekeleza jukumu lake la kutoa mafunzo yenye tija yatakayosaidia kuimarisha ufanisi wa taasisi za elimu na mifumo ya usimamizi wa maarifa, nyaraka na taarifa. Alisisitiza kuwa mafunzo yatakayotolewa yatazingatia mahitaji halisi ya sekta ya elimu kulingana na mabadiliko ya kiteknolojia na sera za kitaifa. Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa ADEM, Dkt. Maulid Maulid, alisema kuwa mkataba huo utaongeza wigo wa ADEM katika kufikia Watendaji wa Elimu wengi zaidi kupitia mafunzo shirikishi yatakayojumuisha masuala ya uongozi, utawala bora, usimamizi wa taasisi za elimu na maendeleo ya rasilimali watu. Aliongeza kuwa ushirikiano na SLADS utaimarisha ubora wa mafunzo kwa kutumia utaalamu wa pande zote mbili. Hafla ya utiaji saini ilishuhudiwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Mhe. Shaibu Ndemanga, ambaye aliipongeza SLADS na ADEM kwa hatua hiyo muhimu akibainisha kuwa uwekezaji katika mafunzo na maendeleo ya rasilimali watu ni msingi wa maendeleo endelevu ya sekta ya elimu na taifa kwa ujumla. Viongozi wengine walioshuhudia tukio hilo ni Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha SLADS ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB), Dkt. Mboni Ruzegea, Mkurugenzi Mkuu wa zamani wa TLSB Prof. Alli Mcharazo, Mkuu wa zamani wa Chuo cha SLADS Dkt. Alfred Nchimbi, Mkurugenzi wa Uendeshaji Huduma za Maktaba wa TLSB Dkt. Rehema Ndumbaro pamoja na Menejimenti ya TLSB na SLADS. Zoezi la utiaji saini wa mkataba huo lilisimamiwa na Wanasheria kutoka TLSB na ADEM ili kuhakikisha makubaliano hayo yanazingatia misingi ya kisheria na maslahi ya pande zote mbili. Kupitia mkataba huu, SLADS na ADEM wanatarajiwa kuanza mara moja utekelezaji wa programu mbalimbali za mafunzo zitakazochangia kuongeza ufanisi wa Watendaji wa Elimu, kuboresha utoaji wa huduma katika sekta hiyo na kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuinua ubora wa elimu nchini.