SLADS YAFANYA KONGAMANO KUKUTANISHA ‘ALUMNAE’
24 Apr, 2025
Chuo cha Ukutubi na Uhifadhi Nyaraka (SLADS) kwa mara ya kwanza kimewakutanisha Wahitimu wa Chuo hicho (Alumnae) katika Kongamano lililofanyika tarehe 22 Novemba 2024, katika viwanja vya SLADS Bagamoyo, Mkoani Pwani.
Mgeni Rasmi katika Kongamano hilo ni Mwenyekiti wa Baraza la Chuo na Mkurugenzi Mkuu wa TLSB Dkt. Mboni Ruzegea.
Katika hotuba yake, Dkt. Ruzegea alianza kwa kuwashukuru Wahitimu hao kwa kuitikia wito wa kushiriki kongamano hilo la kwanza na la kihistoria tangu kuanzishwa kwa Chuo cha SLADS miaka 35 iliyop mapana ya chuo na ita, huku akiushukuru uongozi wa Chuo kwa kuanzisha kongamano hilo lenye manufaa mapana kwa SLADS, wahitimu na tasnia ya Ukutubi kwa ujumla.
Dkt. Ruzegea ameongeza kuwa, Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania ambayo ndio mmiliki wa Chuo cha SLADS, wako tayari kupokea na kufanyia kazi mawazo chanya yatakayowezesha Chuo kujiendesha kwa tija na kufikia malengo ya kuanzishwa kwake.
“Kwa faida ya Alumnae napenda kuwapa taarifa kuwa mnamo mezi Juni, 2023 ofisi ya Mkurugenzi Mkuu kwa kushirikiana na Mkuu wa Chuo waliunda kamati maalum iliyopewa jukumu la kutoa ushauri kuhusu namna bora ya uendeshwaji na usimamizi wa Chuo. Miongoni mwa mapendekezo yaliyotolewa na kamati hiyo ilikua ni kuruhusu makusanyo ya Chuo kutumika katika utekelezaji wa shughuli zake jambo ambalo tayari limeshafanyiwa kazi” ameeleza Dkt. Ruzegea.
Aidha, ameongeza kuwa, kwasasa chuo kinatumia mapato yake yote kuijiendesha, lakini pia kwa kutambua majukumu mengi ya chuo,TLSB imeamua kukigawia Chuo sehemu ya fedha kwa ajili ya matumizi ya ofisi (OC) ili kupunguza ugumu katika uendeshaji wake.
Kwa upande mwingine ameeleza kuwa, mapendekezo mengine yaliyotolewa na kamati hiyo ni pamoja na Chuo kuwa na Muundo wake wa kiuongozi unaojitosheleza, Chuo kuwa ‘Sub – institution’ badala ya ‘Cost Centre’ na kuwezesha malipo kufanyika Chuoni Bagamaoyo ambapo mapendekezo yote yameshafanyiwa kazi.
Dkt. Ruzgea alimalizia kwa kuwataka ‘Alumnae’ kusherehekea mafanikio ya pamoja kwani ni ushuhuda wa elimu waliyoipata chuoni,kujenga mitandao ya kitaaluma na kuchangia maendeleo ya Chuo chao hasa ukizingatia changamoto ya Ukosefu wa vifaa vya TEHAMA vya kujifunzia.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Chuo Bi. Bertha Mwaihojo, alieleza historia fupi ya Chuo cha SLADS tangu kuanzishwa kwake mwaka 1989 mpaka sasa, kozi zitolewazo chuoni hapo, masuala ya Udahili na idadi ya wahitimu tangu kuanzishwa kwake mpaka sasa ambapo ni wahitimu 12,601.
Vilevile, aliongeza kuwa, kwasasa chuo kinakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo; ukosefu wa vifaa vya TEHAMA kufuatia ongezeko la wanafunzi wanaodahiliwa chuoni hapo, Maktaba ndogo, uchakavu wa majengo ya chuo, ofisi za waalimu na Ukumbi wa Mcharazo. Hivyo akawaomba ‘Alumnae’ kuchangia vifaa vya TEHAMA katika maabara ya Chuo hicho.
Kwa upande wao wahitimu wa SLADS ‘Alumnae’ wameushukuru uongozi wa TLSB na SLADS kwa kuwakutanisha kwenye kongamano hilo la kihistoria ambalo litatumika kama jukwaa la kuwakutanisha mara kwa mara kujadilia masuala ya kikutubi na Fani ya Ukutubi kwa ujumla. Vile vile ni jukwaa tosha kujadili maendeleo na mustabali wa SLADS kwa kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.
Aidha, katika Kongamano hilo walichaguliwa viongozi wa muda ambao ni Mwenyekiti na Mwenyekiti Msaidizi, Katibu na Katibu Msaidizi pamoja na Mweka Hazina.
Mwishoni mwa Kongamano hilo, kulifanyika harambee kwa ajili ya kuchangia vifaa mbalimbali kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya kufundishia na Chuo ikiwemo; Kompyuta za mezani 10, kompyuta mpakato 1, Mifuko ya Saruji 61, Mapazia 13 na ahadi za fedha TZS 1,900,000 na USD 100.
Kongamano hilo la Alumnae lilihudhuriwa pia na Wakuu wa Chuo wastaafu ambao ni; Ndug. Hassan Nsubuga (1995 - 2001), Ndug. Zuberi Khatibu (2012 - 2017), Dkt. Alfred Nchimbi (2022 - 2023) na Kaimu Mkuu wa Chuo Bi. Victoria Kessy (2017 - 2022) pamoja na watumishi wa SLADS na TLSB.