Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania

TLSB Logo TLSB Logo
Tafuta kwenye kwa
WAANDISHI WA FASIHI YA KISWAHILI WASISITIZWA KUTUMIA MAKTABA KUONGEZA UMAHIRI
29 May, 2025
service image
Waandishi wa fasihi ya Kiswahili wametakiwa kujenga utamaduni wa kutembelea maktaba ili kupata maarifa mapya na kufahamu mahitaji ya wasomaji wa vitabu kulingana na muktadha wa wakati na mabadiliko ya teknolojia. Wito huo umetolewa na Dkt. Rehema Ndumbaro, Mkurugenzi wa Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB), aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu, Dkt. Mboni Ruzegea, katika Tamasha la Fasihi za Kiswahili msimu wa Tatu lililoandaliwa na Tanzania Fasihi Fund (TAFF)  lililofanyika tarehe 28–29 Mei 2025 katika Kijiji cha Makumbusho, Dar es Salaam. Tamasha hilo lilikuwa na kaulimbiu: “Rudisha Kitabu Nyumbani’’. Dkt. Ndumbaro alisisitiza umuhimu wa waandishi kusajili kazi zao kwa kutumia namba tambuzi za kimataifa za ISBN na ISSN ili kuongeza utambulisho na upatikanaji wa kazi zao katika soko la kitaifa na kimataifa. Aidha, alieleza kuwa TLSB ina jukumu la kuhifadhi, kuendeleza na kusimamia machapisho na kudumisha utamaduni wa usomaji nchini. “Ni muhimu vitabu vifikishwe katika maktaba zetu ili viweze kusambazwa katika maktaba za jamii na kutumika kama rasilimali ya maarifa kwa jamii nzima,” Dkt.Ndumbaro alisema. Dkt. Ndumbaro pia alisema kuwa TLSB itaendelea kushirikiana na taasisi ya Tanzania Fasihi Fund (TAFF) pamoja na wadau mbalimbali wa maktaba ili kuhakikisha kila Mtanzania  hususani wale walioko nje ya miji  wanapata fursa ya kusoma na kujifunza kupitia fasihi ya Kiswahili.  Alibainisha pia kuwa maktaba mtandao itazinduliwa hivi karibuni ili kuongeza upatikanaji wa vitabu kwa njia ya kidijitali. Kwa upande wake, Mkurugenzi wa TAFF, Bw. Hussein Wamaiya, aliwashukuru wadau wote waliojitokeza kushiriki tamasha hilo, akisema kuwa limekuwa sehemu muhimu ya juhudi za kukuza fasihi ya Kiswahili na kuwahamasisha waandishi kushirikiana na jamii katika kuendeleza utamaduni wa kusoma. Washiriki wa tamasha hilo walitembelea gulio la vitabu, kujionea kazi mbalimbali za fasihi za waandishi wa sasa na wale waliotangulia mbele za haki bado kazi zao zinasomwa na kuenziwa. Aidha tuzo mbalimbali zilitolewa kwa washindi ikiwemo ya msomaji Bora iliyokabidhiwa na Dkt,Ndumbaro huku washindi 11 walioandika kuhusu umuhimu wa bima walikabidhiwa tuzo na vyetIi,ambao ni Joyce Mwakajonga mshindi wa kwanza aliyeandika kitabu chenye jina la Hazina, Maimuna Hashim mshindi wa ameandika Kibaruani na Edwin Omindo mshindi watatu kutoka nchini Kenya  aliyeandika Kiburi si Maungwana. Tamasha hilo lilihudhuriwa na waandishi wa vitabu, washairi, wanafunzi, na wadau mbalimbali wa lugha ya Kiswahili, na lililenga kukuza fasihi ya Kiswahili pamoja na kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa usomaji.