Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania

TLSB Logo TLSB Logo
Tafuta kwenye kwa
TLSB YASHIRIKI MAADHIMISHO YA MIAKA 10 YA KAKAMA
16 Feb, 2026
service image
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimeeleza matumaini makubwa waliyonayo kwa Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki (KAKAMA) katika kuimarisha, kukuza na kueneza matumizi ya lugha ya Kiswahili ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na katika ngazi ya kimataifa. Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mgeni Rasmi katika maadhimisho ya miaka kumi ya kuanzishwa kwa KAKAMA, Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla, katika hafla iliyofanyika tarehe 14 Februari 2026, katika Hoteli ya Golden Tulip Zanzibar. Akizungumza katika hafla hiyo, Mheshimiwa Abdulla aliwasilisha salamu za pongezi kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi. Mheshimiwa Abdulla amesema kuwa maadhimisho hayo ni fursa muhimu ya kufanya tathmini ya mafanikio yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwa Kamisheni hiyo mwaka 2016, hususan katika kukuza matumizi ya lugha ya Kiswahili miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Amesisitiza kuwa ni wajibu wa nchi wanachama kuimarisha mabaraza ya Kiswahili katika ngazi za kitaifa ili kuhakikisha lugha hiyo inaendelea kukua, kuimarika na kutumika kikamilifu katika nyanja zote za maendeleo. Aidha, ameeleza kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi zote zinazolenga kukuza, kuendeleza na kulinda lugha ya Kiswahili, ikiwa ni sehemu ya urithi wa kitamaduni na nyenzo muhimu ya utangamano wa kikanda. Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Abdulla amepongeza uamuzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) wa kukitambua Kiswahili kuwa miongoni mwa lugha rasmi za kazi kuanzia Novemba 2025. Amesema hatua hiyo ni ushahidi wa hadhi ya juu iliyofikiwa na lugha ya Kiswahili kimataifa na inapaswa kuwa chachu ya kuendelea kukitumia Kiswahili katika majukwaa ya kimataifa, kitaaluma na kidiplomasia. Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa KAKAMA, Dkt. Caroline Asiimwe, amesema Kamisheni itaendelea kushirikiana na nchi wanachama katika kupanua matumizi ya Kiswahili katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, sayansi, teknolojia na majukwaa ya kidijitali. Amesisitiza kuwa Kiswahili kina nafasi kubwa ya kuwa lugha ya maarifa, ubunifu na maendeleo endelevu endapo kitawekewa mikakati madhubuti ya matumizi. Maadhimisho ya miaka kumi ya KAKAMA yalihudhuriwa na viongozi wa kitaifa na kikanda, mawaziri, mabalozi, wakuu wa taasisi za umma na binafsi pamoja na wadau wa lugha ya Kiswahili. Miongoni mwa viongozi waliohudhuria ni Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB), Dkt. Mboni A. Ruzegea. Katika maadhimisho hayo, msisitizo mkubwa uliwekwa katika utekelezaji wa mikakati madhubuti ya kuendeleza lugha ya Kiswahili kwa kuzingatia kauli mbiu ya maadhimisho isemayo: “Muongo wa KAKAMA, Kuimarisha Utangamano, Ubunifu na Maendeleo Endelevu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.” Sambamba na maadhimisho hayo, yalifanyika maonesho ya taasisi mbalimbali za umma na zisizo za umma, yakilenga kuonesha mchango wao katika kukuza, kudumisha na kuenzi lugha ya Kiswahili. Miongoni mwa taasisi za umma zilizoshiriki maonesho hayo ni Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB). Katika banda la TLSB, huduma mbalimbali zilitolewa ikiwa ni pamoja na huduma za usomaji wa machapisho yaliyoandikwa kwa lugha ya Kiswahili, maonesho ya vitabu vya Kiswahili vilivyoandikwa kabla na baada ya Uhuru, utoaji wa huduma za Maktaba Mtandao Jumuishi ya Kitaifa kwa waandishi, wachapishaji, watafiti na umma kwa ujumla. Aidha, TLSB ilitumia fursa hiyo kutangaza Sheria ya Amana kwa waandishi na wachapishaji pamoja na kutoa huduma za utoaji wa namba tambulishi za vitabu (ISBN) na majarida (ISSN). Pia, TLSB iliandaa mabango yenye jumbe zinazoelezea mchango wake katika kukuza, kuendeleza na kudumisha lugha ya Kiswahili, sambamba na vipeperushi vilivyogawiwa kwa wananchi waliotembelea banda hilo. Vilevile, Mkurugenzi Mkuu wa TLSB alifanya mahojiano na vyombo mbalimbali vya habari vikiwemo TBC1, TBC Online, ZBC, Azam TV, ITV, Gazeti la Daily News, Zanzibar Leo pamoja na Blog Online, ambapo alieleza kwa kina dhamira ya TLSB katika kuenzi na kukuza lugha ya Kiswahili kupitia huduma za maktaba na uhifadhi wa machapisho. Kwa ujumla, maonesho na maadhimisho ya miaka 10 ya KAKAMA yameiwezesha TLSB kujitangaza, kuimarisha taswira yake kwa umma na kuonesha kwa vitendo mchango wake mkubwa katika kukuza, kuendeleza na kuenzi lugha adhimu ya Kiswahili, ambayo ni nguzo muhimu ya utamaduni, elimu na maendeleo ya jamii.