TLSB YAFANYA MAFUNZO YA VVU, UKIMWI, RUSHWA NA AFYA YA AKILI KWA WATUMISHI TLSB
24 Apr, 2025
Bodi ya Huduma za Maktaba Tanazania (TLSB), imefanya Semina kuhusu VVU, Ukimwi, Rushwa na Afya ya Akili kwa Watumishi ili kuwaongezea uelewa, maarifa na njia za kukabiliana na changamoto zitakazojitokeza katika mazingira yao ya kazi. Semina hiyo imefanyika leo tarehe 21 Januari, 2025 katika Ukumbi Mkuu wa Mikutano TLSB Makao Makuu, Dar es Salaam.
Akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Uendeshaji Huduma za Maktaba TLSB (akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu) Dkt. Rehema Ndumbaro, ameishukuru Idara ya Rasilimali watu na Utawala TLSB kwa kuaandaa Semina hiyo na kuwashukuru Wawezeshaji kwa kuitikia wito wa kutoa mada katika Semina hiyo.
Vilevile, amewataka Watumishi TLSB kusikiliza kwa umakini mada zote zitakazotolewa na kuacha tabia ya kuishi kwa mazoea kwani kujifunza ni jambo endelevu katika kuboresha afya zetu, taasisi, Wizara na taifa kwa ujumla.
“Ni jukumu la kila mtu kuendelea kujifunza na kuwa mdau wa kwanza katika kutokomeza VVU na Ukimwi, Rushwa na kujiepusha na masuala yanayopelekea tatizo la afya ya akili. Hivyo nawasihi kusikiliza mada zote na kushiriki zoezi la hiyari la upimaji litakalofanyika baada ya mafunzo haya” amesema Dkt. Ndumbaro.
Dkt. Ndumbaro ameongeza kuwa, TLSB inaunga mkono juhudi za Serikali katika kutoa elimu juu ya masuala ya VVU, Ukimwi, Magonjwa yasiyoambukiza, Rushwa na Afya ya akili. Hivyo, katika kuunga mkono juhudi hizo, Bodi imekua ikitenga bajeti kila mwaka ili kuwezesha Semina hizo kutolewa kwa Watumishi.
Aidha, ameeleza kuwa TLSB inalo jukumu la kuendelea kukusanya, kuhifadhi na kutoa taarifa juu ya masuala hayo kwa vizazi vya sasa na vizazi vijavyo kupitia mtandao wa maktaba zake kote nchini.
Miongoni mwa Mada zilizowasilishwa katika Semina hiyo ni; Elimu kuhusu VVU, Ukimwi na Magonjwa yasiyoambukiza kutoka kwa Mwezeshaji Dkt. Zainab kutoka TACAIDS/Hospitali ya Mnazi Mmoja, Elimu ya Rushwa na athari zake kwa Watumishi wa Umma iliyotolewa na Bi. Immaculate Ngoti na Herman Malima ambao ni Maafisa kutoka TAKUKURU Wilaya ya Ilala na Afya ya Akili kutoka kwa Mwezeshaji Nuruel Kitomari.
Semina kuhusu VVU, Ukimwi, Magonjwa yasiyoambukiza, Rushwa na Afya ya Akili imeandaliwa na Idara ya Rasilimali watu na Utawala na kuhudhuriwa na Watumishi wa TLSB Makao Makuu, Dar es Salaam.