TLSB YAPOKEA MSAADA WA VIFAA NA MICHEZO KUTOKA SKY MOM YA TAIWAN
24 Apr, 2025
Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB) imepokea msaada wa Kompyuta Mpakato (Laptop) 1, Projekta 2 na michezo aina saba ya watoto kwa ajili ya Divisheni ya Watoto na Shule vyenye thamani ya shilingi za Kitanzania 3,047,220 kutoka taasisi ya SKY MOM ya Taiwan tarehe 17 Septemba, 2024.
Akipokea msaada huo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala Bi. Veneranda Mpaze, ameushukuru Uongozi wa SKY MOM kwa vifaa na michezo mbalimbali walioleta Divisheni ya Watoto na Shule TLSB.
Mpaze amongeza kuwa, TLSB ina mtandao wa Maktaba 43 nchi nzima zikiwemo Maktaba za Mikoa, Wilaya na Tarafa, hivyo, Divisheni za Watoto na Shule katika Maktaba hizo bado zina uhitaji wa vifaa na michezo kwa watoto na kuwaomba SKY MOM kupeleka misaada huko pia.
Kwa upande wake Mwakilishi wa SKY MOM Bi. Szhua Tzeng (Shine) kutoka Taiwan, ameshukuru Uongozi wa TLSB kwa mapokezi mazuri. Vilevile, ameeleza kuwa Vifaa na Michezo hiyo itawasaidia sana watoto kujifunza mambo mbalimbali kwa kutumia teknolojia zilizopo.
Tzeng ameongeza kuwa, lengo la taasisi ya SKY MOM ni kuangaza nuru kwa watu wote na kuifanya dunia kuwa sehemu salama ya kuishi kwa amani na upendo.
Kwa upande mwingine, Kaimu Mkuu wa Divisheni ya Watoto na Shule Bi. Mwajuma Rasuli, ameushukuru Uongozi wa SKY MOM kwa vifaa walivyotoa na kuahidi kuvitunza ili viweze kutumika kwa muda mrefu na kunufaisha watoto wengi.