TLSB YAPOKEA UGENI KUTOKA BARAZA LA WAWAKILISHI ZANZIBAR
28 Apr, 2025
Kamati ya Kudumu ya Ustawi wa Jamii ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Sabiha Filfil Thani, imefanya ziara katika ofisi za Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB) Makao Makuu jijini Dar es Salaam, tarehe 14 Agosti, 2024.
Akimuwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TLSB katika kikao na kamati hiyo mara baada ya mapokezi, Mkurugenzi wa Uendeshaji Huduma za Maktaba Dkt. Rehema Ndumbaro, ameeleza kuwa TLSB imekuwa ikafanya kazi nyingi kwa ushirikiano na Bodi ya Huduma za Maktaba Zanzibar (ZLSB) ili kuwawezesha Wananchi wa Tanzania Bara na Visiwani kunufaika kwa pamoja na Huduma za Maktaba nchini.
Dkt. Ndumbaro ameongeza kuwa, TLSB inatoa huduma za Maktaba kwa watu wote kupitia mtandao wa Maktaba zake nchini ikiwemo; Maktaba za Mikoa 22, Wilaya 19 na Tarafa 2, sambamba na Maktaba ya Wasioona iliyopo Shule ya Uhuru Mchanganyiko jijini Dar es Salaam.
Aidha, ameeleza kuwa TLSB inatoa pia mafunzo ya Ukutubi na Uhifadhi Nyaraka kupitia Chuo cha Ukutubi na Uhifadhi Nyaraka (SLADS), chenye Makao yake Makuu Bagamoyo mkoani Pwani na kampasi ya Dar es Salaam iliyopo Ofisi za Maktaba Kuu ya Taifa Posta.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Ustawi wa Jamii ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe. Sabiha Filfil Thani, ameeleza lengo la kutembelea TLSB ni kubadilishana mawazo na kuona namna bora ya uendeshaji wa Maktaba ili kuendana na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia na kuweza kuishauri Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali ya Zanzibar juu ya maboresho ya miundombinu katika Sekta ya Elimu.
“Rais wa Zanzibar ameipa umuhimu sekta ya elimu kwa kuipa kipaumbele katika utekelezaji wa shughuli zake, hivyo ni muhimu kupata fursa ya kutembelea miradi mbalimbali na kujifunza wenzetu TLSB wanafanya nini”. Mhe. Sabiha Filfil Thani ameeleza.
Dkt. Ulfat A. Ibrahim ni miongoni mwa Viongozi kutoka Zanzibar walioongozana na kamati hiyo. Akiongea katika kikao hicho, Dkt. Ulfat ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Huduma za Maktaba Zanzibar (ZLSB), amesema kuwa ZLSB itaendelea kushirikiana na TLSB katika kuboresha utoaji wa huduma za Maktaba nchini kwani TLSB imekua na mchango mkubwa kwa Waandishi ikiwemo utoaji wa namba za Utambulisho kwa Vitabu (ISBN) na Majarida (ISSN).
Kwa upande mwingine, Mwakilishi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Evaristo Mtitu, amewaeleza Wanakamati kuwa Wizara (WyEST), imeanza mchakato wa kukusanya maoni kutoka kwa Wadau wa Elimu na Wananchi wa jinsia zote, na taaluma mbalimbali. Mchakato huo utawezesha Wizara kuandaa Sera itakayoongoza Maktaba zote nchini.
Awali kabla ya kikao hicho, Kamati ilipata wasaa wa kuzunguka katika Idara, Vitengo na Divisheni mbalimbali ndani ya Maktaba Kuu ya Taifa, ikiwemo Kitengo cha Maktaba Mtandao.
Kamati ya Kudumu ya Ustawi wa Jamii ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Sabiha Filfil Thani imeambatana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Dkt. Khalid Masoud Waziri, Mkurugenzi wa Bodi ya Huduma za Maktaba Zanzibar Dkt. Ulfat A. Ibrahim, Mwakilishi kutoka WyEST Dkt. Evaristo Mtitu na Afisa Elimu wa Mkoa wa Dar es Salaam Ndug. Gift Kyando.