Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania

TLSB Logo TLSB Logo
Tafuta kwenye kwa
TLSB YASHIRIKI MAONESHO KATIKA SHEREHE ZA ROMBO MARATHON & NDAFU FESTIVAL 2025
31 Dec, 2025
service image
Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB) imeshiriki kikamilifu katika Maonesho yaliyofanyika sambamba na Sherehe za Rombo Marathon & Ndafu Festival 2025, zilizofanyika tarehe 23 Desemba, 2025 katika Viwanja vya Michezo vya Msitu wa Rongai (Rongai Forest Sports Grounds) vilivyopo Tarakea, Wilaya ya Rombo, Mkoa wa Kilimanjaro. Ushiriki wa TLSB katika maonesho hayo ni sehemu ya mkakati wa Bodi wa kuendelea kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa kusoma, matumizi ya maktaba za kisasa na kidijitali, pamoja na upatikanaji wa maarifa na taarifa sahihi kwa maendeleo ya mtu binafsi na taifa kwa ujumla. Kupitia jukwaa hilo, TLSB ililenga kuwafikia wananchi wa Wilaya ya Rombo na maeneo ya jirani kwa kutoa elimu, huduma na ushauri wa kitaaluma unaohusiana na huduma za maktaba. Sherehe hizo zilihudhuriwa na Mgeni Rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Nurdin Babu, aliyeongozana na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda, ambaye pia ni miongoni mwa viongozi wa Bodi ya Rombo Marathon & Ndafu Festival. Vilevile, sherehe hizo zilishuhudiwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, taasisi za umma na binafsi, pamoja na wananchi wengi waliokusanyika kushiriki katika tukio hilo la kijamii, michezo na utamaduni. Kupitia banda la TLSB, wananchi walipata fursa ya kunufaika na huduma mbalimbali ikiwemo: Uandikishaji wa wanachama wapya wa maktaba, kwa watu binafsi, shule na taasisi mbalimbali; Utoaji wa namba za utambulisho wa vitabu na majarida (ISBN na ISSN) kwa waandishi, wachapishaji na taasisi; Huduma za usomaji wa vitabu na magazeti, kwa lengo la kukuza na kuendeleza utamaduni wa kusoma katika jamii; Utoaji wa elimu kuhusu mafunzo ya Ukutubi na Uhifadhi wa Nyaraka yanayotolewa kupitia Chuo cha Sayansi ya Maktaba na Nyaraka (SLADS); Huduma za Maktaba Mtandao (Digital Library Services) zinazowezesha upatikanaji wa taarifa na maarifa kwa njia ya kidijitali. Katika tukio la mbio za Rombo Marathon & Ndafu Festival, viongozi wa TLSB walioshiriki kukimbia umbali wa Kilomita 5 ni pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa TLSB, Dkt. Mboni Ruzegea, Mkurugenzi wa Uendeshaji Huduma za Maktaba, Dkt. Rehema Ndumbaro, Kaimu Meneja wa Rasilimali Watu na Utawala, Ndug. Kenedy Nsenga, pamoja na Mkutubi wa Mkoa wa Arusha, Bi. Rafiki Kilonzo. Baada ya kukamilisha mbio hizo, viongozi hao walitunukiwa medali kama ishara ya ushiriki wao katika tukio hilo. Aidha, watumishi wa TLSB walioshiriki kutoa huduma na elimu kwa wananchi ndani ya banda la maonesho ni Msimamizi wa Maktaba za Mikoa, Bi. Nikobiba Kigadye, Afisa Habari na Mawasiliano, Bi. Veronica Bisendo, Mkutubi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Bi. Sakina Msuya, Mkutubi wa Maktaba ya Tarafa ya Mbweera, Ndug. Paschal Tarimo, pamoja na Mkutubi kutoka Maktaba ya Mkoa wa Kilimanjaro, Bi. Christina Masue. Kupitia ushiriki wake katika Rombo Marathon & Ndafu Festival 2025, TLSB imeendelea kudhihirisha dhamira yake ya kutumia majukwaa ya kitaifa na kijamii kuelimisha umma kuhusu mchango wa maktaba katika kukuza elimu, utafiti, ubunifu na maendeleo endelevu ya jamii, sambamba na kuhamasisha matumizi ya rasilimali za taarifa zinazopatikana kupitia maktaba za kisasa na za kidijitali.