Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania

TLSB Logo TLSB Logo
Tafuta kwenye kwa
TSLB YAPOKEA VITABU KUTOKA JUMUIYA YA KIISLAM YA AHMADIYYA
23 Apr, 2025
service image
Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB) imepokea vitabu vyenye maudhui mbalimbali zaidi ya 20 kutoka kwa Jumuiya ya Kiislam ya Ahmadiyya ukanda wa Mnazi Moja mkoa wa Dar es Salaam, tarehe 24 Januari 2024. Miongoni mwa mwa vitabu vilivyopokelewa vina maudhui kama vile; Quran tukufu, Hadithi za Mtume Muhammad S.A.W, Masomo ya Kiislam (Maswali na Majibu), Maisha ya Mtume Muhammad S.A.W na vingine vingi. Akipokea vitabu hivyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TLSB, Mkurugenzi wa Idara ya Uendeshaji wa Maktaba Dkt. Rehema Ndumbaro, ameishukuru Jumuiya ya Ahmadiyya kwa mchango wa vitabu huku akisisitiza jukumu kubwa la TLSB katika kufikia umma wa Watanzania.  “Kwasasa tuna jukumu kubwa la kuwahudumia umma, na nyie mmekuwa wadau wakubwa, hivyo tunashukuru sana kwa mchango huu wa vitabu kwani Maktaba ni nyumba ya maarifa ambapo watu wa dini zote, Sheikh, Askofu na wengine wengi wanaitumia kujipatia taarifa na maarifa mbalimbali”. Kwa upande wake Sheikh wa Ahmadiyya Mkoa wa Dar es Salaam Sheikh Nadeem Ahmed, amesema kuwa kazi kubwa wanaoifanya ni kusambaza maarifa na elimu kwa watu wote na dini zote. Vilevile, wamekua wakichapisha vitabu vinne (4) mpaka vitano (5) kwa Mwaka na kusambaza kwa watu na taasisi mbalimbali. Aidha, ameahidi kuleta machapisho hayo TLSB ikiwemo jarida la Mapenzi ya Mungu wanalochapisha kila mwezi. Kwa upande mwingine, Rais wa Ahmadiyya ukanda wa Mnazi mmoja Ndug. Mohamed Yunus Haji ameishukuru TLSB kwa mapokezi mazuri na kupewa nafasi ya kufanya maonesho yao ya vitabu ambapo walinufaika kuuza baadhi ya vitabu na machapisho. Naye Mwalimu wa Ahmadiyya ukanda wa Mnazi mmoja Mwl. Adam Msekwa, amesema kuwa mafundisho yote ya Dini ya Kiislam ya Ahmadiyya yanaeleza kuwa Islam ni dini ya amani, na imekua ikitafsiri machapisho na vitabu mbalimbali vya dini ya Kiislam kwa lugha ya Kiswahili ili watu wote waweze kuelewa, huku akitoa mfano wa Quran Tukufu iliyotafsiriwa kwa mara ya kwanza na Ahmadiyya mwaka 1953. Aidha ameongeza kuwa, msikiti wa Mnazi mmoja umekua kitovu cha kuandika mashairi na ulichangia sana katika harakati za kupigania Uhuru ambapo Mwalimu Julius K. Nyerere aliutumia sana Msikiti huo kwa vikao na kukutana na watunzi wa mashairi na kupanga mikakati mbalimbali ya ukombozi wa Tanganyika. Dini ya Kiislam ya Ahmadiyya ilianza rasmi mwaka 1889 na Makao yake Makuu yalikua nchini India, baadae yalihamia Pakistan. Kwasasa Makao Makuu yapo nchini Uingereza chini ya Kiongozi Mkuu Khafatul Masih V. Mirza Masroor Ahmad Atba.