Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania

TLSB Logo TLSB Logo
Tafuta kwenye kwa
UFUNGUZI WA MAKTABA YA MKOA WA RUVUMA
31 Dec, 2025
service image
Serikali imeonesha kwa vitendo kwamba Maktaba ni nyenzo muhimu ya kupunguza pengo la maarifa, kuongeza usawa wa fursa na kujenga uchumi wa kisasa wa viwanda, ubunifu na TEHAMA. Hayo yemesemwa tarehe 03 Desemba, 2025 na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma na Mgeni Rasmi Mhe. Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed  katika Hafla ya Ufunguzi wa Maktaba ya Mkoa wa Ruvuma iliyofanyika katika viwanja vya Maktaba hiyo. Brigedia Jenerali Ahmed ameongeza kuwa Maktaba si jengo tu, bali ni nyumbani kwa maarifa, mahali pa kuamsha fikra, kuibua ubunifu, kufanya utafiti na kuongeza maarifa yanayohitajika katika dunia ya leo. Hivyo, amewataka wanafunzi, vijana, walimu na wadau wa elimu kutumia maktaba hiyo kama fursa ya kukuza ubunifu, utafiti na mawazo mapya. Awali akitoa neno fupi kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Songea Mhe. Kapenjama  Ndile, ameitaka TLSB kuwa na vitabu na machapisho yenye kuakisi hali halisi ya jamii husika, huku akielezea uhitaji wa machapisho yanayoelezea Ziwa Nyasa na aina ya samaki wanaopatikana katika ziwa hilo na shughuli za uchimbaji wa makaa ya Mawe ili kuwezesha jamii kupata taarifa sahihi na kuweza kujikwamua kimaisha. Naye Kaimu Mwenyekiti wa Bodi Prof. Kelefa Mwantimwa amesema kuwa Maktaba ni Kitovu cha Maarifa na ujuzi, hivyo, uwepo wa Maktaba ni muhimu kwa mustakabali wa maendeleo ya jamii yeyote ile. Awali Mkurugenzi Mkuu wa TLSB Dkt. Mboni Ruzegea, akiwasilisha taarifa ya ukarabati wa Maktaba ya Mkoa wa Ruvuma ameeleza kuwa, Bodi imefanya ukarabati huo kwa takribani miaka mitatu hadi kukamilika kwake huku akiongeza kuwa bado kuna uhitaji wa Vifaa vya TEHAMA ili kuwezesha watumiaji wa Maktaba kupata huduma za maktaba kimtandao. Dkt. Ruzegea alitumia pia jukwaa hilo kuelezea mafanikio ya Bodi yaliyopatikana katika kipindi cha Miaka 5 iliyopita ikiwemo uanzishwaji wa Maktaba Mtandao Jumuishi ya Kitaifa, ukarabati wa Miundombinu ya Maktaba na ununuzi wa Vitabu vyenye maudhui ya ndani kwa fedha zilizotengwa na serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Vilevile, ujenzi wa Maktaba ya kumbukumbu ya Hayati John Pombe Magufuli wilayani Chato na Maktaba ya Mkoa wa Mwanza.