VIJANA WATAKIWA KUTUMIA AKILI UNDE KUKUZA TALANTA ZAO
20 Nov, 2025
Vijana nchini wametakiwa kujenga mazoea ya kutumia maktaba katika enzi hii ya
mabadiliko na kukua kwa teknolojia hasa Akili Unde, ili kujiongezea ujuzi unaohitajika
katika dunia ya sasa.
Hayo yamesemwa tarehe 19 Novemba, 2025 na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya huduma
za Maktaba Tanzania, Dkt. Mboni Ruzegea katika mkutano na waandishi wa habari
uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa TLSB, Posta Dar e Salaam ikiwa ni
maandalizi ya kuelekea Maonesho ya 32 ya Vitabu ya Kimataifa Tanzania
yaliyoandaliwa na Chama cha Wachapishaji Tanzania (PATA) kwa kushirikiana na
TLSB.
Dkt. Ruzegea amesema maktaba ni kitovu cha maarifa, hivyo rasilimali za elimu kutoka
fani mbalimbali hukusanywa ili kuwawezesha vijana kupata taarifa sahihi pamoja na
fursa za kugundua na kukuza vipaji vyao. Aliwahimiza vijana kufika maktaba na kutumia
huduma za kisasa zinazotolewa ili kuongeza ujuzi unaohitajika katika dunia ya sasa
yenye mabadiliko ya kasi ya kiteknolojia.
Aidha, amewataka waandishi wa vitabu kuendelea kuzalisha kazi bora zinazoendana
na mabadiliko ya teknolojia, akibainisha kuwa Tanzania ina waandishi wengi wenye
uwezo mkubwa na wanaochangia katika kuhifadhi historia na utamaduni wa taifa kupitia
machapisho.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wachapishaji Tanzania (PATA), Bw.
Hermes Damian, amesema maonesho ya vitabu yanatoa fursa kwa waandishi kuelezea
mawazo, uzoefu na hisia zao mbele ya dunia. Alisisitiza umuhimu wa jamii kukuza
utamaduni wa kusoma, ikiwemo familia kuwa na vitabu na kumsomea mtoto angalau
kitabu kimoja kwa wiki.
Bw. Hermes aliongeza kuwa historia na utambulisho wa Mwafrika umehifadhiwa na
kuenezwa kwa kiasi kikubwa kupitia vitabu, hivyo wachapishaji wana jukumu muhimu la
kulinda na kuendeleza hazina hiyo ya maarifa.
Amesema maonesho ya mwaka huu yanatarajiwa kushirikisha nchi mbalimbali duniani
pamoja na Jumuiya ya Wachapishaji Afrika (African Publishers Network), hatua
inayodhihirisha ushirikiano mpana wa kimataifa katika sekta ya uchapishaji.
Naye Katibu wa PATA, Bw. Abdallah Saiwaad, amesema kutakuwepo na mashindano
ya usomaji kwa watoto, mabanda ya wachapishaji kutoka ndani na nje ya nchi, pamoja
na mauzo ya vitabu kwa bei ya punguzo ili kuongeza upatikanaji wa vitabu kwa
wananchi wengi zaidi.
Maonesho hayo yatafanyika kuanzia Novemba 21 hadi 26, 2025, yakiongozwa na
kaulimbiu:
“Vitabu ni Hifadhi ya Maarifa na Utamaduni.”


