Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania

TLSB Logo TLSB Logo
Tafuta kwenye kwa
WAANDISHI WATAKIWA KUANDIKA VITABU VYENYE MAUDHUI YA KITANZANIA
19 Jul, 2025
service image
Waandishi na watunzi wa vitabu wametakiwa kuandika maudhui yanayoakisi maisha halisi na utamaduni wa Mtanzania, ili kuendeleza na kuimarisha urithi wa taifa kupitia maandiko. Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Maktaba nchini, Dkt. Rehema Ndumbaro aliyemuwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TLSB, katika hafla ya uzinduzi wa vitabu vitano vya watoto vilivyochapishwa na kampuni ya Mtalimbo, iliyofanyika tarehe 18 Julai, 2025, katika ukumbi wa Maktaba Kuu ya Taifa jijini Dar es Salaam. Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Dkt. Ndumbaro amesema kuwa Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB) inaendelea na juhudi za kueneza maarifa kwa jamii kwa kununua vitabu na kuvisambaza katika maktaba za jamii zilizopo na zile zitakazoanzishwa kote nchini. Aidha, amewashauri waandishi wa vitabu kuweka alama ya umri unaofaa kwa kila kitabu, ili kusaidia wazazi na walezi kuwachagulia watoto wao vitabu vinavyolingana na hatua zao za ukuaji na maendeleo ya kielimu. Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kampuni ya uchapishaji ya Mtalimbo, Bw. Hussein Wamaywa, ameishukuru TLSB kwa ushirikiano wao katika kuhakikisha maarifa yanawafikia Watanzania. Pia amepongeza juhudi za TLSB katika utoaji wa namba za ISBN na uhifadhi wa vitabu hivyo kwa matumizi ya baadaye. Vitabu vilivyozinduliwa ni pamoja na; Nani Mzuri – kimeandikwa na Bi. Amina A. Mohamed (Zanzibar), Babu Yangu Anajua Kila Kitu – Mwamwimgila Goima (Mtalimbo Books),Mfalme Mwamatoki – Christopher Zakaria,Rafiki Yangu Kipepeo – Hussein Wamaywa na Tumaini – Riziki Mohamed Juma (Zanzibar) Vitabu hivyo vyote ni vya watoto na vina maudhui yanayolenga kuongeza uelewa, maarifa, na kupanua fikra za watoto katika mazingira ya Kitanzania. Uzinduzi huo umehudhuriwa na waandishi wa vitabu, watunzi, wachapishaji, wasomaji na wasambazaji wa vitabu kutoka sehemu mbalimbali.