WAKUTUBI WATAKIWA KULINDA NA KUHIFADHI KUMBUKUMBU ZA TAIFA KATIKA ENZI YA TEKNOLOJIA
31 Dec, 2025
Wakutubi nchini wametakiwa kuhifadhi, kulinda na kusimamia taarifa pamoja na kumbukumbu za Taifa kwa weledi na uadilifu mkubwa, kwani taaluma yao ni muhimu sana katika ulimwengu wa sasa unaokabiliwa na kasi kubwa ya maendeleo ya teknolojia.
Wito huo umetolewa tarehe 20 Desemba, 2025 na Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo ambaye pia alikuwa Mgeni Rasmi, Mhe. Shaibu Ndemanga, wakati wa Mahafali ya 31 ya Chuo cha Ukutubi na Uhifadhi Nyaraka (SLADS) yaliyofanyika katika Hoteli ya Stella Maris, Bagamoyo, mkoani Pwani.
Akizungumza katika mahafali hayo, Mhe. Ndemanga alisema kuwa katika mazingira ya sasa ya kidijitali, Wakutubi wamebeba jukumu zito la kuwa walinzi wa taarifa na kumbukumbu muhimu za taasisi na Taifa kwa ujumla. Alisisitiza kuwa taaluma ya ukutubi ni nguzo muhimu ya maendeleo ya kijamii, kiutamaduni na kiuchumi.
“Katika ulimwengu huu ambapo teknolojia inakua kwa kasi sana, Mkutubi ni mlinzi wa taarifa na kumbukumbu. Mmebeba mzigo mzito, na naamini mtaenda kuitendea haki taaluma yenu,” alisema Mhe. Ndemanga.
Aidha, aliitaka Sekta ya Elimu nchini kuangalia upya mitaala pamoja na Sera ya Elimu ili kukabiliana na changamoto ya ajira kwa Wakutubi, huku akisisitiza umuhimu wa uwepo wa Wakutubi katika Maktaba za Shule za Msingi, Sekondari na Vyuo vya Amali nchini.
Akizungumza kwa niaba ya Chuo, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha SLADS ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB), Dkt. Mboni Ruzegea, alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kwa kuendelea kuipatia TLSB fedha za matumizi mengineyo na fedha za maendeleo. Alieleza kuwa sehemu ya fedha hizo tayari zimeanza kutumika kuboresha miundombinu ya Chuo cha SLADS.
Dkt. Ruzegea pia aliomba Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo kushirikiana na Chuo hicho kwa kuwezesha wanafunzi wa SLADS kupata maeneo ya kufanya mafunzo kwa vitendo (field attachment) ndani ya Wilaya hiyo, ili kuwaandaa zaidi kwa mazingira halisi ya kazi.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Kamishna wa Elimu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia anayeshughulikia Masuala ya Maktaba na Kiswahili, Dkt. Maryam Mwinyi, aliwataka wahitimu kutumia elimu waliyoipata chuoni hapo kama nyenzo ya maendeleo binafsi na ya Taifa, na kuzingatia maadili ya taaluma yao.
Naye Kaimu Mkuu wa Chuo cha SLADS, Bi. Bertha Mwaihojo, aliwasilisha taarifa ya Chuo iliyojumuisha historia ya SLADS, mafanikio yaliyopatikana pamoja na changamoto zinazoendelea kukikabili Chuo hicho. Miongoni mwa changamoto alizozitaja ni uhaba wa kumbi za mihadhara na kukosekana kwa uzio wa Chuo, hali inayosababisha changamoto za kiusalama kwa wanafunzi, wafanyakazi na mali za Chuo.
Awali, katika risala yao, Wahitimu wa Mahafali ya 31 ya SLADS waliiomba Serikali kuzingatia uwezekano wa kuwawezesha mikopo ya fedha kwa kada ya Ukutubi na Uhifadhi Nyaraka ili kuwapa fursa zaidi za kujikwamua kiuchumi.
Katika Mahafali hayo, jumla ya Wahitimu takribani 135 walitunukiwa Stashahada ya Ukutubi na Uhifadhi Nyaraka, tayari kujiunga na soko la ajira na kuchangia maendeleo ya sekta ya elimu na Taifa kwa ujumla.
Chuo cha Ukutubi na Uhifadhi Nyaraka kinaendelea kujizatiti katika kutoa mafunzo bora, kuimarisha miundombinu na kushirikiana na wadau mbalimbali kwa lengo la kukuza na kuendeleza taaluma ya Ukutubi na Uhifadhi Nyaraka nchini.


