WAKUTUBI WATAKIWA KUTUMIA TEKNOLOJIA ZA KISASA KATIKA KUCHAKATA, KUTAYARISHA NA KUHIFADHI TAARIFA
24 Apr, 2025
Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) Dkt. Maulid J. Maulid amewataka Wakutubi kujifunza na kutumia teknolojia za kisasa katika kuchakata, kutayarisha na kuhifadhi taarifa.
Dkt. Maulid ameyasema hayo katika Mahafali ya thelathini (30) ya Chuo cha Ukutubi na Uhifadhi Nyaraka (SLADS) yaliyofanyika tarehe 23 Novemba 2024 katika Hoteli ya Stella Maris, Wilayani Bagamoyo mkoani Pwani, ambapo alikua Mgeni Rasmi akimwakilisha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Adolf Mkenda. Katika Hotuba yake, Dkt. Maulidi amewataka Wahitimu kujiendeleza zaidi kitaaluma kwa teknolojia za kisasa ili kutekeleza majukumu yao kwa wakati na ufanisi unaohitajika.
“Kwenu Wahitimu, safari ya kujifunza haijaishia hapa, tumieni maarifa mliyoyapata kwa vitendo. Mna jukumu la kujifunza teknolojia za kisasa ili mtekeleze majukumu yenu kuendana na mahitaji ya ulimwengu wa sasa”. Amesema Dkt. Maulid.
Dkt. Maulid ameongeza kuwa, SLADS ina jukumu la kuandaa mitaala itakayowezesha wanafunzi kujifunza teknolojia zilizopo ili kuendana na hali halisi ya sasa na kuweza kujiajiri, pia ameahidi kutafuta namna bora ya ADEM na SLADS kushirikiana katika programu mbalimbali na kubadilishana uzoefu. Aidha, amesema kuwa, Serikali inatambua kwamba elimu, sayansi na teknolojia ni injini ya taifa, hivyo, itaendelea kuimarisha miundombinu ya Chuo, huku akiahidi kupeleka changamoto zote kwa Waziri Mkenda kwa utatuzi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Chuo na Mkurugenzi Mkuu wa TLSB Dkt. Mboni Ruzegea, amesema kuwa fani ya Ukutubi ni fani kongwe iliyoanza tangu Karne ya tatu, huku akielezea mipango ya kuboresha Huduma za Maktaba nchini ambayo tayari imeshaanza ikiwemo; maboresho ya Sheria ya TLSB, uundaji wa Sera ya Huduma za Maktaba nchini, uanzishaji wa Maktaba Mtandao na uboreshaji wa utolewaji wa huduma hizo. Aidha Dkt. Ruzegea ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuikumbuka TLSB kwenye miradi mbalimbali huku akiomba pia ikumbukwe kwenye Mradi wa HEET.
Kwa upande mwingine Makamu Mkuu wa Chuo cha SLADS Bi. Bertha Mwaihojo amemshukuru Mgeni Rasmi kwa ujio wake, huku akielezea changamoto mbalimbali zinazokikabili chuo hicho kama vile; Uchache wa Madarasa na ofisi za waalimu hasa ukizingatia kuanzishwa kwa kozi mpya chuoni hapo, Uhaba wa Vifaa vya kujifunzia vya Tehama na Ukosefu wa vyombo vya usafiri.
Nao Wahitimu katika risala yao wamemshukuru Mgeni Rasmi kwa kushiriki pamoja nao katika mahafali hayo huku wakielezea changamoto zinazowakabili ikiwemo, uchakavu wa miundombinu ya madarasa, ukosefu wa mabweni, chumba kidogo cha Maktaba ya chuo, uhaba wa vitabu, na ukosefu wa vifaa vya kujifunzia vya Tehama.
Mahafali ya thelathini ya SLADS yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Wilaya ya Bagamoyo, Wakuu wa Vyuo na shule jirani, Watumishi wa TLSB na SLADS, Wazazi na wageni mbalimbali. Jumla ya Wahitimu 172 wametunukiwa Stashahada ya Ukutubi na Uhifadhi Nyaraka katika Mahafali hayo.