Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania

TLSB Logo TLSB Logo
Tafuta kwenye kwa
WANAFUNZI WA GOSHENI NURSERY AND PRIMARY SCHOOL WATEMBELEA MAKTABA KUU YA TAIFA
24 Oct, 2025
service image
Wanafunzi 48 wa Shule ya Msingi na Awali ya Gosheni iliyopo Bunju ‘A’, wilaya ya Kinondoni, wamefanya ziara ya mafunzo katika Maktaba Kuu ya Taifa Posta, leo tarehe 24 Oktoba 2025, jijini Dar es Salaam. Wageni hao walipokelewa na Bi. Rosemary Joseph, ambaye ni Mkutubi wa Kitengo cha Watoto, na aliwaongoza kutembelea vitengo mbalimbali vya Maktaba. Wakiwa hapo, walipata maelezo kuhusu huduma zinazotolewa na Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB), ikiwemo usajili wa machapisho, utoaji wa namba za ISBN na ISSN, pamoja na utunzaji wa machapisho ya waandishi wa Kitanzania katika Kitengo cha Bibliografia ya Taifa (NBA). Vilevile , walitembelea Kitengo cha Ufundi (TSD), ambako machapisho huchakatwa kabla na kusambazwa katika maktaba za TLSB nchini, pamoja na Kitengo cha Usomaji kwa Watu Wazima (RSD), walikopata elimu kuhusu huduma kwa wasomaji na uazimashaji wa vitabu ndani ya Maktaba. Ziara hiyo ilihitimishwa katika Kitengo cha Watoto, ambapo wanafunzi walipata fursa ya kusoma vitabu mbalimbali vya hadithi na riwaya, kuimba nyimbo za shule, na kushiriki michezo ya kielimu iliyopo katika kitengo hicho. Kwa upande wake, Kiongozi wa ziara hiyo, Bi. Maimuna Said, aliishukuru TLSB kwa mapokezi mazuri na elimu waliyoipata wanafunzi hao. “Ziara hii imewapa wanafunzi wetu hamasa ya kupenda kusoma na kuelewa umuhimu wa maktaba katika kuhifadhi maarifa ya taifa.” Alisema Bi.Maimuna. Aidha, wanafunzi hao 48 wakiwa na walimu watatu pamoja na mkutubi wa maktaba ya shule ya Gosheni, walipata nafasi ya kujionea machapisho yaliyohifadhiwa kabla na baada ya Uhuru, jambo lililoongeza uelewa wao kuhusu historia na urithi wa kitaifa