WATUMISHI WANAWAKE TLSB WAHIMIZWA KUNYANYUANA KATIKA MAENEO YA KAZI ILI KULETA MAENDELEO KWA TAIFA
24 Apr, 2025
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB) Dkt. Mboni Ruzegea amewahimiza wanawake kunyanyuana katika maeneo ya kazi na kwingineko ili kujiletea maendeleo kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Dkt. Ruzegea ameyasema hayo hii leo tarehe 8 Machi, 2024 katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambapo Watumishi wanawake wa TLSB wameungana na wanawake wengine kote Duniani kuadhimisha siku hii muhimu kwao.
Akizungumza sambamba na kauli mbiu ya mwaka huu isemayo "Wekeza kwa Wanawake Kuharakisha Maendeleo ya Taifa na Ustawi wa Jamii", Dkt. Ruzegea amesema;
"Huwezi kuwekeza kwa wanawake na kuharakisha maendeleo kama mwanamke mwenzako yuko chini, msikubali kuona wenzetu walioko chini hawapandi juu, na mtu wa kwanza kumnyanyua mwanamke mwenzake ni mwanamke mwenyewe." Amesema Dkt. Ruzegea
Aidha, ameongeza kuwa mchango wa mwanamke haupaswi kusherehekewa katika siku moja tu kwa mwaka bali ni kila sekunde, dakika, saa, siku, juma, mwezi na mwaka. Vilevile, amesisitiza wanawake kupendana, kuwa na umoja, na kuoneana huruma pindi mmoja anapopata tatizo.
Dkt. Ruzegea pia amepata wasaa wa kufurahi na Watumishi wanawake wa TLSB kwa kuimba nyimbo za hamasa kuhusu masuala ya wanawake na baadae kukata na kuwalisha keki wanawake waliohudhuria hafla fupi iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano TLSB Makao Makuu, Dar es Salaam.
Mbali na hafla hiyo fupi, Watumishi wanawake TLSB wameungana na wanawake wengine wa jiji la Dar es Salaam na viunga vyake katika maadhimisho ya kilele cha siku ya Wanawake Duniani kimkoa yaliyofanyika katika uwanja wa Mji Mwema, Wilaya ya Kigamboni, Jijini Dar es salaam.
Mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho hayo kwa ngazi ya Mkoa ni Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila.
Katika hotuba yake, Mhe. Chalamila amesema wanawake wanapitia changamoto mbalimbali wakiwa makazini na hata nyumbani, hivyo, maadhimisho hayo huwaleta pamoja wanawake kutambua mchango na uwezo wao kazini na nyumbani.
"Mwanamke ni tabibu, huleta tabasamu na furaha ambayo ni tiba, mwanamke ni mbunifu, mwanamke ni Afisa Uhusiano ambaye anaunganisha familia na jamii kwa ujumla ". Amesema Mhe. Chalamila.
Mhe. Chalamila amewataka wanawake wasikate tamaa, wasiruhusu dharau, bali waoneshe vipaji na uwezo wao wakiwa kazini na nyumbani huku akisisitiza elimu kwa mtoto wa kike.
Aidha, amewataka wanawake kuondokana na hofu na kushiriki katika uongozi ikiwemo kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali katika siasa na watambue wana nafasi muhimu katika kulijenga taifa.
Siku ya Wanawake Duniani huadhimishwa kila tarehe 8, Machi ya kila mwaka ili kutambua mchango wa wanawake katika nyanja mbalimbali duniani kote.