UFUNGUZI WA MAONESHO YA 33 YA KIMATAIFA YA VITABU TANZANIA
12 Oct, 2026
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma, na Mgeni Rasmi, leo tarehe 12 Octoba 2026 alifungua Maonesho ya 33 ya Kimataifa ya Vitabu Tanzania, katika viwanja vya Maktaba Kuu ya Taifa jijini Dar es Salaam.
Maonesho hayo yameandaliwa na Chama cha Wachapishaji Tanzania (Publishers Association of Tanzania – PATA).
Katika Hotuba yake, Mhe. Naibu Waziri amesisitiza umuhimu wa kulinda hakimiliki na kuendeleza usomaji. Pia alielezea umuhimu wa sekta ya vitabu nchini katika kuchaingia elimu, ubunifu na uhifadhi wa historia ya taifa.
Aidha, amesema kuna haja ya kukuza lugha ya Taifa ya Kiswahili kwa serikali kushirikiana na wadau mbalimbali zikiwemo, taasisi za umma na binafsi, waandishi, wachapishaji na wasomaji.
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB), Dkt. Mboni Ruzegea, ambaye pia ni mwenyeji wa Maonesho hayo, amesema Serikali kupitia Bodi ya Huduma za Maktaba itaendelea kununua vitabu vyenye maudhui ya ndani (local content) kutoka kwa waandishi na wachapishaji wa Kitanzania, ili kukuza soko la vitabu na kuongeza ufikishiaji wa vitabu hivyo kwa Umma.
Dkt Ruzegea alielezea huduma zitolewazo na Bodi kwa Wachapishaji na Waandishi wa vitabu ikiwemo utoaji wa namba za kimataifa za utambulisho wa vitabu (ISBN) nchini, katika mfumo unaoratibiwa na International ISBN Agency.
Alisema Bodi kupitia kitengo cha Bibliografia ya Taifa huorodhesha na kuyahifadhi machapisho ya vitabu kwa ajili kurahisi tafiti mbalimbali na uhifadhi kwa vizazi vijavyo, na taarifa za wachapishaji nchini hujumuishwa katika Global Register of Publishers kupitia Maktaba ya Taifa ambae ni wakala wa kitaifa wa ISBN.
Dkt. Ruzegea amewaalika waandishi na wachapishaji kujiunga na mfumo Jumuishi wa Maktaba Mtandao ya Taifa Taifa (INDLS) ili vitabu viweze kuwafikia wananchi wengi zaidi na alisema Bodi itazingatia hakimiliki na maslahi yao katika usomaji mtandaoni.
Naye Mwenyekiti wa PATA, Bw. Hermes Damian, aliiomba serikali kuendelea kutambua juhudi za waandishi na alipendekeza kuwepo kwa Sera ya Taifa ya Vitabu na Usomaji na kuwa shule ziwezeshwe kisera kununua vitabu vya Kiswahili chini ya uratibu wa Bodi, ili kuongeza maarifa kwa watoto na kupanua soko la vitabu. Pia, ameomba Serikali kujenga Maktaba ya Kitaifa ya Kiswahili kwa ajili ya uhifadhi wa kazimbalimbali za uandishi na sanaa zilizo katika lugha ya Kiswahili.


