KONGAMANO LA NNE LA KITAIFA KUHUSU HUDUMA ZA MAKTABA TAMASHA LA VITABU NA USOMAJI
21 Sep, 2026
TLSB YAANDAA KONGAMANO LA NNE LA KITAIFA KUHUSU HUDUMA ZA MAKTABA, TAMASHA LA VITABU NA USOMAJI
Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB) inayo furaha kuwaalika kwenye Kongamano la Nne la Kitaifa kuhusu Huduma za Maktaba, Tamasha la Vitabu na Usomaji, litakalofanyika kuanzia tarehe 20–22 Oktoba 2026 katika viwanja vya Maktaba Kuu ya Taifa, Posta, jijini Dar es Salaam.
Mgeni Rasmi katika Kongamano hilo anatarajiwa kuwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda.
Mada Kuu ya Kongamano ni:
“Maboresho ya Huduma za Maktaba kupitia Mageuzi ya Kidijitali, Kukuza Maarifa na Ujuzi kwa Maendeleo Endelevu.”
Kongamano hili litawakutanisha wadau mbalimbali, wakiwemo wataalamu wa habari na taarifa, wanazuoni, wakutubi, wadau wa elimu, waandishi na wachapishaji, washirika wa maendeleo, taasisi za umma na binafsi, pamoja na viongozi mbalimbali.
Uzinduzi wa Mfumo Jumuishi wa Maktaba Mtandao ya Taifa (iNDLS)
Miongoni mwa matukio muhimu katika Kongamano la mwaka huu ni uzinduzi rasmi wa Mfumo Jumuishi wa Maktaba Mtandao ya Taifa (iNDLS), ambao unatarajiwa kuwa hatua muhimu katika mageuzi ya kidijitali ya huduma za maktaba nchini Tanzania.
Mfumo wa iNDLS unalenga kuwezesha upatikanaji wa rasilimali za maktaba na taarifa kupitia majukwaa ya kidijitali, hivyo kusaidia ujifunzaji, utafiti, ubadilishanaji wa maarifa na ukuzaji wa ujuzi kwa wananchi.
Maonesho ya Vitabu na Mashindano ya Usomaji
Kongamano hilo pia litakuwa na maonesho ya vitabu, yatakayowapa waandishi, wachapishaji, taasisi na wadau wengine wa elimu fursa ya kuonesha na kutangaza vitabu pamoja na rasilimali mbalimbali za habari, taarifa na maarifa.
Aidha, kutakuwa na mashindano ya usomaji kwa watoto na wanafunzi, ambapo washindi watapatiwa zawadi kwa kutambua na kuhamasisha ushiriki na uwezo wao katika usomaji.
Washiriki pia watapata fursa ya kufurahia burudani kutoka kwa wasanii na vikundi mbalimbali.
Hivyo, TLSB inawakaribisha wataalamu wa habari na taarifa, wanazuoni, wakutubi, wadau wa elimu, waandishi, wachapishaji, taasisi za umma na binafsi, wanafunzi, watoto na wananchi kwa ujumla kushiriki katika tukio hili muhimu la kitaifa.
Jiunge nasi tarehe 20–22 Oktoba 2026 katika viwanja vya Maktaba Kuu ya Taifa, Posta, jijini Dar es Salaam, tunaposherehekea vitabu, usomaji, maarifa na mageuzi ya kidijitali katika huduma za maktaba.
NYOTE MNAKARIBISHWA!
#MaktabaKidijitaliNaUjuziKwaDira2050


