Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania

TLSB Logo TLSB Logo
Tafuta kwenye kwa
MAHAFALI YA 32 YA SLADS: NDEMANGA AWATAKA WAHITIMU KUENDANA NA MAGEUZI YA KIDIGITALI
27 Nov, 2026
service image
Mgeni rasmi katika Mahafali ya 32 ya Chuo cha Ukutubi na Uhifadhi Nyaraka (SLADS), Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Mhe. Shaibu Ndemanga, amewataka wahitimu wa chuo hicho kuongeza kasi katika matumizi ya teknolojia katika shughuli zao ili kuendana na mageuzi ya kidijitali yanayoendelea nchini na duniani kwa ujumla. Mhe. Ndemanga ameyasema hayo tarehe 26 Novemba, 2026, katika mahafali ya 32 ya chuo hicho yaliyofanyika Hoteli ya Stella Maris, Bagamoyo, Mkoa wa Pwani, akieleza kuwa matumizi ya teknolojia ni hali halisi ya sasa inayotokana na mageuzi na maendeleo ya kidijitali, hivyo wahitimu wanapaswa kuendana nayo katika utekelezaji wa majukumu yao. Aidha, Mhe. Ndemanga amesema Wilaya ya Bagamoyo kwa sasa ina kasi ya ujenzi wa viwanda, hivyo amevitaka vyuo vilivyopo wilayani humo kuhakikisha vinatatua changamoto zinazokabili viwanda hivyo kwa kuwapatia wataalamu mbalimbali. Amebainisha kuwa viwanda hivyo vimeajiri vijana wengi wanaomaliza elimu ya vyuo vya kati pamoja na wataalamu wa masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA). Pia, amewataka wahitimu kwenda kuwa wabunifu, wazalendo na wenye kujituma katika majukumu yao, akisisitiza kuwa Serikali inawahitaji sana vijana wenye sifa hizo katika kuchangia maendeleo ya Taifa. Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB), Mhe. Balozi Prof. Elizabeth Kiondo, ameeleza kuwa Chuo cha SLADS kipo chini ya Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB) na kilianza rasmi kutoa mafunzo ya Ukutubi na Uhifadhi Nyaraka mwaka 1989. Mhe. Balozi Prof. Kiondo amesema TLSB imeanza kutekeleza Mpango Mkakati wa miaka mitano (2026/2027–2030/2031), ambapo kupitia mpango huo changamoto nyingi zinazokikabili chuo, hususan masuala ya taaluma na miundombinu, zinatarajiwa kutatuliwa ili kuimarisha mazingira ya utoaji wa mafunzo na maendeleo ya chuo. Naye Mwenyekiti wa Baraza la Chuo na Mkurugenzi Mkuu wa TLSB, Dkt. Mboni Ruzegea, ameiomba Serikali kutoa fursa za ajira kwa wahitimu wa SLADS katika masuala ya Ukutubi, hususan kuajiriwa katika maktaba za shule na vyuo. Amesema wahitimu hao wana ujuzi na uwezo zaidi katika nafasi hizo kuliko walimu ambao hawana ujuzi wa masuala ya maktaba, lakini wamepewa jukumu la kusimamia maktaba katika maeneo hayo. Aidha, Dkt. Ruzegea ameongeza kuwa Baraza la Chuo linaunga mkono mageuzi yanayofanyika chuoni hapo, hususan katika maboresho ya mitaala, miundombinu na mafunzo, ili kuhakikisha wakufunzi wanakuwa wataalamu na kuwafundisha wanafunzi kwa weledi, hatua itakayochangia kufikia Dira ya Taifa ya 2050. Awali, katika taarifa yake, Kaimu Mkuu wa Chuo cha SLADS, Bi. Bertha Mwaihojo, ameishukuru Serikali kwa kutenga kiasi cha shilingi milioni 572 kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya chuo. Aidha, amesema chuo kimeingia makubaliano na ADEM kwa ajili ya kushirikiana katika utoaji wa mafunzo ya muda mfupi yatakayowasaidia wakufunzi kunufaika na mafunzo hayo. Nao wahitimu, kupitia risala yao kwa mgeni rasmi, wameomba chuo kufanyiwa maboresho ya miundombinu ya madarasa na ukumbi wa chuo, masjala na maktaba, pamoja na kuwezeshwa kupata vifaa vya kujifunzia na kufundishia. Vilevile, wameahidi kuwa mabalozi wazuri wa chuo hicho katika maeneo watakayokwenda kufanya kazi na kuendeleza majukumu yao. Katika mahafali hayo, jumla ya wanafunzi 129 wamehitimu, ambapo wanafunzi 61 wamehitimu Stashahada ya Ukutubi na Usimamizi wa Taarifa, huku wanafunzi 68 wakihitimu Stashahada ya Utunzaji Kumbukumbu na Usimamizi wa Nyaraka. Kwa sasa, Chuo cha SLADS kinatoa kozi nne ambazo ni Stashahada ya Ukutubi na Usimamizi wa Taarifa, Stashahada ya Utunzaji Kumbukumbu na Usimamizi wa Nyaraka, Stashahada ya TEHAMA na Stashahada ya Uongozi wa Biashara. Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB) inaendelea kuimarisha utoaji wa elimu na mafunzo kupitia SLADS kwa lengo la kuzalisha wataalamu wenye ujuzi, weledi na uwezo wa kukabiliana na mahitaji ya soko la ajira na kuchangia maendeleo ya Taifa.  

slot gacor