Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania

TLSB Logo TLSB Logo
Tafuta kwenye kwa
MWENYEKITI WA BODI TLSB AIPONGEZA MENEJIMENTI KWA MAENDELEO YA MFUMO WA iNDLS, AAGIZA UPANUZI WA HUDUMA KATIKA MAKTABA 43 NCHINI
15 Oct, 2026
service image
Dar es Salaam, 15 Oktoba 2026 Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB) Mhe. Balozi Prof. Elizabeth Kiago Kiondo, ameipongeza Menejimenti ya Bodi hiyo kwa juhudi zinazofanyika katika kuendeleza Mfumo Jumuishi wa Maktaba Mtandao wa Taifa (iNDLS), huku akielekeza kufanyika kwa tathmini ya mfumo huo na kupanua matumizi yake kutoka maktaba 11 zilizopo sasa hadi kufikia maktaba zote 43 za TLSB nchini. Mwenyekiti ametoa maelekezo hayo Oktoba 15, 2026, wakati wa ziara yake katika ofisi za TLSB Makao Makuu, Posta Dar es Salaam, ambapo amepata fursa ya kufahamishwa shughuli zinazotekelezwa na Idara na Vitengo mbalimbali vya Bodi, kujionea utendaji kazi wa mfumo wa iNDLS na kutembelea mabanda ya maonesho ya 33 ya chama cha Wachapishaji Tanzania (PATA) yanayoendelea katika viwanja vya Maktaba Kuu ya Taifa. Akizungumza katika kikao na Menejimenti ya TLSB, Prof. Kiondo amesema ziara hiyo imelenga kujionea maendeleo ya shughuli za Bodi na kufahamu juhudi zinazochukuliwa katika kuboresha huduma za maktaba nchini. Amesema ni muhimu kwa Bodi na Menejimenti kuendelea kufuatilia utekelezaji wa majukumu ya Taasisi ili kuhakikisha kuwa shughuli zinazofanyika zinaendana na malengo yaliyowekwa na kuleta matokeo yanayotarajiwa. Akizungumzia mfumo wa iNDLS, Mwenyekiti amepongeza hatua zilizofikiwa, hususan muunganiko wake na mifumo mingine ya Serikali, ikiwemo MUSE, NeST na GAMIS. Ameeleza kufurahishwa na namna mfumo huo unavyowezesha upatikanaji wa taarifa za watumiaji na kurahisisha huduma za usomaji na uazimishaji wa vitabu. Amesisitiza kuwa matumizi ya teknolojia katika huduma za maktaba ni muhimu katika kuongeza ufanisi wa utendaji kazi, kurahisisha upatikanaji wa taarifa na kupanua wigo wa huduma kwa wananchi. Hata hivyo, ameelekeza Bodi kufanya tathmini ya mfumo wa iNDLS tangu ulipoanzishwa hadi sasa ili kubaini mafanikio yaliyopatikana, changamoto zilizojitokeza na maeneo yanayohitaji maboresho. Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuweka mpango wa maendeleo wa miaka mitatu ijayo ili kuhakikisha mfumo huo unakamilishwa na kufanya kazi kwa ukamilifu kulingana na malengo yaliyokusudiwa. Katika hatua nyingine, Mwenyekiti amesisitiza kuwa taarifa zote zinazotakiwa kuingizwa katika mfumo zinapaswa kuwa na malengo na muda maalumu wa kukamilishwa. Amesema ni muhimu kuhakikisha taarifa hizo zinakusanywa, zinaingizwa na kusasishwa kwa wakati ili kuimarisha ufanisi wa mfumo na kuboresha huduma kwa watumiaji wa maktaba. Vilevile, ameitaka Menejimenti kutekeleza majukumu yake kwa weledi na uwajibikaji kwa kuzingatia Mpango Mkakati Mpya wa TLSB wa mwaka 2026/2027–2030/2031. Ameeleza kuwa utekelezaji wa mpango huo unapaswa kuongozwa na dira, dhima na thamani za msingi za Taasisi ili kuhakikisha kuwa kila idara na kitengo kinachangia katika kufikia malengo ya kimkakati. Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uendeshaji Huduma za Maktaba, Dkt. Rehema Ndumbaro, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TLSB, amemshukuru Mwenyekiti wa Bodi kwa ziara hiyo na maelekezo aliyoyatoa kwa lengo la kuimarisha utendaji kazi wa Taasisi. Dkt. Ndumbaro amesisitiza umuhimu wa Menejimenti na watumishi kujiwekea malengo ya kazi kwa vipindi vya wiki, mwezi na mwaka ili kuwezesha ufuatiliaji wa utekelezaji wa majukumu na kuhakikisha malengo yaliyowekwa katika Mpango Mkakati Mpya yanafikiwa. Ameeleza kuwa utaratibu huo utasaidia kupima maendeleo ya kazi, kubaini changamoto mapema na kuchukua hatua stahiki kwa wakati, huku ukihimiza ushirikiano kati ya idara na vitengo vyote vya Taasisi. Katika ziara hiyo, Mwenyekiti wa Bodi pia alipokea taarifa rasmi kuhusu Kongamano la Nne la Kitaifa kuhusu Huduma za Maktaba, Tamasha la Vitabu na Usomaji, ambalo ni jukwaa muhimu la kuwakutanisha wadau wa maktaba, vitabu na usomaji kwa ajili ya kubadilishana uzoefu na kuendeleza utamaduni wa kusoma nchini litakalofanyika kuanzia tarehe 20 – 22 Oktoba 2026. Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za Bodi na Menejimenti za kuimarisha usimamizi wa utekelezaji wa majukumu ya TLSB, kuboresha huduma za maktaba na kuhakikisha wananchi wanapata fursa pana zaidi za kupata maarifa kupitia huduma za maktaba za kisasa.  

slot gacor